Yanga SC yaja na Bacca Day kuiua Al Ahly

KANDANDA Yanga SC yaja na Bacca Day kuiua Al Ahly

Zahoro Mlanzi • 10:00 - 28.11.2023

Huo umekuwa ni utaratibu wa Yanga msimu huu katika mechi za kimataifa kutoka na mchezaji maalumu ambaye anaibeba siku husika.

Timu ya Yanga SC, imezindua hamasa zao visiwani Zanzibar kuelekea mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ambapo mchezo huo umepewa jina la 'Bacca Day'.

Mchezo huo wa hatua ya makundi utafanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam kuanzia saa 1 usiku.

Kuelekea mchezo huo, aliyekabidhiwa rungu ni mlinzi wa kati wa timu hiyo, Ibrahim Abdullah 'Bacca' ambaye ni mchezaji wa kutumainiwa ndani ya kikosi.

Kupitia hasama hiyo Yanga, imeingia mkataba wa wiki moja na taasisi mbili kubwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo itavuna mkwanja wa takribani sh. milioni 40.

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) pamoja na Mamlaka ya Kuhamasisha Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kila mmoja imeweka sh. milioni 20 kwa klabu hiyo.

Tukio la uzinduzi wa hamasa hiyo limehudhuriwa na viongozi wa juu wa Yanga wakiongozwa na Rais wao, Injinia Hersi pamoja na Makamu wake, Arafat Hajji.

Kwa mara ya kwanza katika hamasa za aina hiyo walikuwa na Max Day katika mchezo dhidi ya ASAS ya Djibouti na walishinda kwa mabao 5-1 huku Max Nzengeli mwenyewe akiweka kambani mabao 2.

Katika mchezo mwingine dhidi ya El Marreikh ya Sudan waliupa jina la Key Day ambapo ilikuwa ni kwa ajili ya kiungo wa mshambuliaji, Stephan Aziz Ki.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi cha Yanga, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema timu ipo kambini kwasasa na wachezaji wanajiandaa vya kutosha ili kuwapa raha mashabiki wa Yanga.

Amesema mara tu baada ya kufika nchini, timu ilipewa mapumziko ya muda mchache lakini hadi sasa wachezaji wote wameshakusanyika Avic Town na maaandalizi makali yanaendelea.

Yanga inaingia katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ikiwa imetoka kufungwa ugenini nchini Algeria dhidi ya CR Belouizdad kwa mabao 3-0.