Simba SC yabanwa na Asec Mimosa bao 1-1

KANDANDA Simba SC yabanwa na Asec Mimosa bao 1-1

Na Zahoro Mlanzi • 19:18 - 25.11.2023

Huo ni mchezo wa kwanza wa Kundi B wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu ya Simba SC, imebanwa mbavu nyumbani kwa kulazimishwa sare ya 1-1 na Asec Mimosa ya Ivory Coast.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ni wa kwanza kwa kila timu katika hatua ya makundi.

Simba ndio ilikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 41 likifungwa na Saido Ntibanzokiza kwa mkwaju wa penalti baada ya mlinzi wa Asec kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Asec nao ilisawazisha bao hilo dakika ya 78 ya mchezo, mfungaji akiwa ni Serge Pokou.

Simba ilionekana kuwa bora zaidi katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo mara baada ya kurudi kipindi cha pili, wageni Asec walionekana kuutawala mchezo hadi kusawazisha bao.

Mara baada ya mchezo huo, Simba watasafiri hadi Botswana ambapo Desemba 2 watavaana na Jwaneng Galaxy huku Asec nao wakiwawakiribisha Wydad Casablanca ya Morocco katika mfululizo wa mechi za Kundi B.

Kwa ujumla, timu za Tanzania hazijaanza vizuri katika michuano hiyo baada ya kuwashuhudia Yanga wakipoteza mchezo wao wa ugenini dhidi ya CR Belouizdad kwa mabao 3-0.