Yanga SC yaanza vibaya makundi Afrika

KANDANDA Yanga SC yaanza vibaya makundi Afrika

Zahoro Mlanzi • 07:33 - 25.11.2023

Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kushika mkia kutoka Kundi D la michuano hiyo ikiwa haina alama

Timu ya Yanga SC, imeanza vibaya hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

Licha ya kutawala mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Julai 5 nchini humo kwa vipindi vyote, Yanga imeshindwa kuifungua safu ya ulinzi ya wapinzani wao ambao muda mwingi walikuwa nyuma ya mpira.

Mabao mawili ya Belouizdad, yamefungwa katika dakika 45 za kwanza kupitia kwa Raouf Benguit na Abderrahmane Meziane.

Benguit amefunga bao la kwanza katika dakika 10 za kwanza baada ya kukutana na mpira uliokolewa vibaya na mabeki wa Yanga na kuujaza wavuni.

Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga ilijipanga na kufanya mashambulizi ya nguvu ambapo kwa nyakati tofauti Max Nzengeli na Mudathir Yahya walipiga mashuti nje ya eneo ambayo yalipanguliwa na Kipa, Alexis Guendouz na kuwa kona iliyokosa madhara.

Katika dakika 3 za nyongeza kipindi cha kwanza, Meziane alifunga bao la pili akimalizia krosi ya Oussama Darfalou.

Kipindi cha pili, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, alifanya mabadiliko kwa kumtoa Mudathir Yahya na kuingia Clement Mzize.

Mabadiliko hayo yalionekana kuleta uhai katika safu ya ushambuliaji ya Yanga lakini tatizo lilikuwa kuivuka safu ya ulinzi ya Belouizdad.

Zikiwa zimeongezwa dakika 4 kufikia dakika 90, straika Lamin Jallow alifunga bao la tatu ambalo liliimaliza Yanga.

Yanga sasa itakuwa na kibarua kigumu ambapo itaialika Al Ahly ya Misri katika mchezo mwingine wa Kundi D utakaopigwa Desemba 2 Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.