Yanga yaomba ufafanuzi kufungiwa Aucho

LIGI KUU Yanga yaomba ufafanuzi kufungiwa Aucho

Zahoro Mlanzi • 20:06 - 20.11.2023

Amefungiwa michezo mitatu baada ya kuonesha utovu wa nidhamu wakati wa mechi dhidi ya Coastal Union.

Klabu ya Yanga, wametuma barua kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutaka ufafanuzi kuhusu adhabu ambayo amepewa kiungo wao, Khalid Aucho ya kufungiwa mechi tatu.

Aucho amefungiwa michezo mitatu ikiwa ni baada ya tukio la Novemba 8 wakati wa mchezo wa ligi hiyo baina ya wenyeji Coastal Union na Yanga ambapo kiungo huyo alionekana kumpiga kiwiko Ibrahim Ajib.

Kutokana na tukio hilo aliyekuwa Mwamuzi wa kati, Emmanuel Mwandembwa, alimuonya Aucho kwa kadi ya njano lakini bodi hiyo iliamua kumpa Aucho adhabu ya ziada huku mwamuzi akifungiwa miezi 6.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema wanachofanya sio kukata rufaa bali ni kuomba tu ufafanuzi wa kikanuni kuhusu adhabu hiyo.

Amesema hapo awali baadhi ya matukio ambayo sio mazuri yalitokea dhidi yao na hata walipojaribu kutuma barua kwenda bodi ya ligi ili kuomba haki itendeke walijibiwa kuwa hakuna adhabu mara mbili.

"Hatujakata rufaa ila tumeomba ufafanuzi kuhusu hizi adhabu, hapo awali matukio ya namna hii yalitokea kwa wachezaji wetu na tulipofuatilia tuliambiwa hakuna adhabu mara mbili," amesema.

"Sasa hatuelewi hii imekuaje kwa upande wetu na ndio maana tumeomba ufafanuzi," amemalizia Kamwe.

Yanga wanatarajia kumkosa kiungo huyo katika michezo mitatu ya ligi hiyo ambayo itakuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Tabora United na Kagera Sugar.

Mbali na adhabu hizo lakini pia Yanga walitozwa faini ya shilingi milioni 5 kwa kosa la kuingia kupitia mlango ambao sio rasmi katika mchezo wa Novemba 5 dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa Mkapa..

Pia mlinda lango wa Yanga, Djigui Diarra ametozwa faini ya shilingi laki 5 kwa kosa la kushangilia moja kati ya mabao yao mbele ya benchi la ufundi la Simba.