Yanga SC yazindua jezi zenye ujumbe wa Afrika

KANDANDA Yanga SC yazindua jezi zenye ujumbe wa Afrika

Zahoro Mlanzi • 19:05 - 22.11.2023

Jezi zilizozinduliwa ni za aina tatu ambapo za nyumbani ni rangi ya kijani, ugenini ni rangi ya njano na nyeusi ni ile ya ziada.

Timu ya Yanga SC, imezindua jezi mpya kwa ajili ya michuano ya kimataifa huku zikibeba ujumbe kwa nchi za Afrika.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam huku timu hiyo ikiwa ipo nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad.

Mara baada ya uzinduzi huo, katika mitandao mbalimbali ya kijamii inaonekana kupokelewa vizuri kutokana na walio wengi kupongeza kwa jinsi zilivyotengenezwa.

Jezi zilizozinduliwa ni za aina tatu ambapo za nyumbani ni rangi ya kijani, ugenini ni rangi ya njano na nyeusi ni ile ya ziada.

Katika jezi hizo, zina maneno ya maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika hivyo kibiashara inawezwa kuuzika katika nchi yoyote ya Afrika.

Katika hatua nyingine, wachezaji ambao walikuwa wakiitumikia timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', iliyokuwa ikicheza na Morocco katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, wameungana na wenzao nchini Algeria baada ya kuondoka alfajiri ya leo.

Wachezaji hao ni Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Nickson Kibabage, Ibrahim Abdullah, Aboutwalib Mshery na Mudathir Yahya.

Mchezo huo utapigwa Ijumaa saa nne usiku katika Uwanja wa Julai 5 ambao waliutumia katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger msimu uliopita