Chama, Kapama mguu nje, ndani Mapinduzi Cup

KANDANDA Chama, Kapama mguu nje, ndani Mapinduzi Cup

Zahoro Mlanzi • 17:06 - 26.12.2023

Nyota hao wa timu ya Simba SC walisimamishwa tangu Desemba 21 na hadi sasa hakuna kikao kilichofanyika kujadili hatma yao

Wakati pazia la michuano ya Mapinduzi Cup 2023, likitarajiwa kufunguliwa Alhamisi, wachezaji Clatous Chama na Nassor Kapama, bado hawajui hatma yao ndani ya timu ya Simba SC baada ya kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

Michuano hiyo itafunguliwa kwa kuchezwa mechi kati ya bingwa mtetezi, Mlandege FC itakayoumana na Azam FC, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar. Simba SC yenyewe imepangwa Kundi B na Singida FG, Jamhuri SC na APR ya Rwanda

Akizungumza jijini Dar es Salaam kuhusu hatma ya wachezaji hao, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema taarifa kamili kuhusu wachezaji hao itatolewa kama ilivyotolewa awali wakati wanafungiwa.

Hata hivyo Ally amesema wachezaji hao wote bado ni sehemu ya timu yao na wanapata stahiki zao zote kama wachezaji wengine na aliahidi kuwa hivi karibuni mbivu na mbichi zitabainika.

"Kwasasa kumekuwa na ratiba nyingi ambazo pia zimeandamana na sikukuu hivyo bado kamati haijakaa, lakini wote wawili ni wachezaji wetu na jambo likikamilika tutawapa taarifa," amesema.

Chama na Kapama wamesimamishwa na uongozi wa Simba tangu Desemba 21, kutokana na kile ambacho kilidaiwa ni utovu wa nidhamu. Hata hivyo bado haijabainishwa kosa gani walilofanya.

Wachezaji hao hawakuwa sehemu ya mchezo wakati timu hiyo ilivyoshuka uwanjani kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC, Desemba 23 ambapo Simba walibanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya 2-2 katika Uwanja wa Azam Complex.

Chama amekuwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi muhimu cha Simba kwa kipindi chote alichokuwa na timu tangu alipojiunga kwa mara ya kwanza mwaka 2018.

Hata hivyo hali si shwari kwa Kapama ambaye tangu alipojiunga na Simba mwanzo wa msimu uliopita akitokea Kagera Sugar nafasi ya kucheza imekuwa ngumu na hajaonekana uwanjani katika mechi yoyote ya mashindano msimu huu.

Katika hatua nyingine, Kocha wa Makipa wa timu hiyo, Daniel Cadena, ameibuka na ujumbe ambao unaonekana kuwa na maana tata.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Cadena, ameeleza ni vyema akafanya maamuzi magumu ambayo yatamuumiza lakini yatamuwezesha kusimamia taaluma yake kwa siku za mbele.