Kocha wa Yanga ataka straika mpya wa mabao

KANDANDA Kocha wa Yanga ataka straika mpya wa mabao

Zahoro Mlanzi • 16:52 - 24.12.2023

Hiyo imetokana na hadi sasa mabao mengi ya timu hiyo yanafungwa na viungo washambuliaji huku mastraika waliopo wanaonekana hawana msaada

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesemaanahitaji straika mpya katika dirisha dogo la usajili.

Hayo amesema mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam wakitokea Dodoma ambapo Jumamosi walicheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United na kushinda 1-0.

Gamondi amesema wao kama timu kubwa siku zote wanaangalia fursa ya kujiimarisha kwenye kikosi chao.

"Timu yetu ni kubwa kama zilivyo timu nyingine kubwa duniani, tunaangalia nafasi ya kuboresha timu kila nafasi inapopatikana," amesema.

Amesema kwasababu wanaingia katika mzunguko wa pili wanatarajia ushindani mkubwa hivyo wataongeza wachezaji katika nafasi tofauti ikiwemo ushambuliaji.

Yanga wanashika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo wakiwa na alama 30 nyuma ya Azam wanaongoza wakiwa na alama 31.

Katika upande wa upachikaji mabao, Yanga hadi sasa pia wanashika nafasi ya pili wakiwa wamefunga mabao 31 nyuma ya Azam wenye mabao 35.

Yanga wanahusishwa na baadhi ya washambuliaji akiwemo Sankara Karamoko wa Asec Mimosa, Jonathan Sowah Medeama SC na Ranga Chivaviro wa Kaizer Chiefs katika dirisha hili la usajili.