Gamondi alia ugumu wa ratiba mwishoni mwa mwaka

KANDANDA Gamondi alia ugumu wa ratiba mwishoni mwa mwaka

Zahoro Mlanzi • 10:53 - 23.12.2023

Kocha huyo wa Yanga anakabiliwa na mtihani huo mgumu kwani timu yake pia itahitajika pia katika michuano ya Mapinduzi Cup itakayoanza Desemba 28

Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema ratiba yao kuelekea mwisho wa mwaka sio nzuri lakini watajitahidi kupambana ili kupata matokeo chanya.

Kauli hiyo ameitoa akiwa mkoani Dodoma wakati kikosi chake kikijiandaa kukabiliana na Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Gamondi amesema ratiba ni ngumu kwasababu wanahitajika kucheza mechi kila baada ya siku tatu kitu ambacho sio rahisi kwa kawaida.

"Ratiba inatubana, tunalazimika kucheza mechi kila baada ya siku tatu, ni ngumu lakini inabidi tupambane ili kupata matokeo mazuri," amesema.

Aidha kocha huyo amebainisha hali ya Uwanja wa Jamhuri ambao watautumia kwa ajili ya mchezo wa dhidi ya Tabora kwamba sio nzuri na haitoi fursa kwa timu yake kucheza soka wanalohitaji.

Katika hatua nyingine, Kocha huyo, amesema kwenye mchezo wa kesho wataendelea kumkosa mchezaji wa Joyce Lomalisa kutokana na majeraha.

Kocha huyo amedai walitarajia Lomalisa angerudi mapema uwanjani lakini hadi sasa anaonekana kutokuwa tayari hivyo nafasi yake itaendelea kuzibwa kikosini hadi atakapokuwa fiti.

Tags: