Straika Lusajo aachana na Namungo FC

KANDANDA Straika Lusajo aachana na Namungo FC

Zahoro Mlanzi • 16:08 - 25.12.2023

Nyota huyo alishawahi kuzichezea timu za Yanga SC na KMC na ni miongoni mwa wachezaji wenye elimu kubwa nchini Tanzania

Straika wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Reliants Lusajo, ameachana na timu ya Namungo FC kwa kuwaaga wachezaji wenzake na mashabiki wao kwa ujumla.

Taarifa ya kuachana na timu yake ameitoa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Timu hiyo ya Namungo inashiriki Ligi Kuu Bara ikitumia Uwanja wa Majaliwa kwa mechi za nyumbani ulioko mkoani Lindi.

Dirisha dogo la usajili tayari limefunguliwa tangu Desemba 16 na wachezaji wanatoka na kuingia kwenye klabu tofauti ambapo ameweka wazi kwamba anakwenda kupata changamoto sehemu nyingine.

Geita Gold na Tabora United zinatajwa kuwa kwenye hesabu za kuiwinda saini ya nyota huyo ambaye ni mshambuliaji.

Katika ujumbe wake huo, Lusajo ameandika; “Napenda Kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Namungo na benchi la ufundi bila kusahau mashabiki wote wa timu ya Namungo kwa kipindi chote tulichokuwa pamoja. Ni muda wangu sasa wa kuangalia changamoto sehemu nyingine. Nipende kuwatakia kila la kheri katika msimu huu wa ligi.”

Ikumbukwe kwamba nyota huyo alirejea kwa mara nyingine ndani ya Namungo 2021 akitokea Klabu ya KMC lakini pia alishawahi kucheza Yanga SC.

Lusajo ni miongoni mwa wachezaji wachache kwenye ligi hiyo ambao wana elimu kubwa kwani ana shahada 'degree' ya Ugavi (Bachelor of Arts in Procurement) aliyoipatia Chuo Kikuu cha Usharika Moshi.