Benchikha asema mambo makubwa yanakuja Simba

KANDANDA Benchikha asema mambo makubwa yanakuja Simba

Na Zahoro Mlanzi • 13:00 - 18.12.2023

Kocha huyo mwenye mataji ya Kombe la Shirikisho Afrika na Super Cup, Jumanne atakuwa uwanjani kuiongoza timu hiyo dhidi ya Wydad Casablanca

Kocha Mkuu wa kikosi cha Simba SC, Abdelhak Benchickha, amesema bado hajaanza kuonesha mpira wake anaotarajia ndani ya timu hiyo.

Mbali na hilo, Benchikha amesema kwasasa muhimu timu inapata matokeo lakini kuhusu kiwango chake anachokitaka bado hakijafikiwa kwa asilimia 100.

Hayo ameyazungumza jijini Dar es Salaam ikiwa zimepita siku mbili tangu alipotoka kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

"Kwasasa bado tunatafuta mzani wa kikosi lakini ushindi wa 3-0 ni mzuri kwa kuanzia, wachezaji wanajitahidi kufanya vizuri lakini kwangu bado naona tuna safari ndefu ya kufikia aina ya mpira ambao nautaka," amesema.

Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu kiwango cha Benchikha tangu alipoanza kazi ya kuifundisha Simba mapema mwezi huu. Watu wengi wanaamini kuwa timu hiyo kwasasa inacheza mpira mkubwa kitu ambacho kocha hajakikubali.

Kocha huyo ameiongoza Simba kwenye mechi mbili muhimu za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi. Mechi zote hizo alikuwa katika uwanja wa ugenini akianza na Jwaneng Galax nchini Botswana na kutoka suluhu na kisha kufungwa 1-0 na Wydad Casablanca ya Morocco.

Benchikha anauzoefu mkubwa na soka la Afrika, msimu uliopita alishinda taji la Shirikisho Afrika akiwa na USM Alger na tayari alishawahi kushinda taji la Super Cup akiwa na Berkane ya Morocco.

Kwasasa anatajwa kuwa ni kocha mwenye mafanikio makubwa zaidi kwenye Ligi ya Tanzania. Kocha huyo anatarajia Jumanne kukiongoza kikosi cha Simba kwenye mchezo wa nyumbani dhidi ya Wydad ambao alama tatu ni muhimu zaidi kwa timu zote.

"Mchezo dhidi ya Wydad ni kama fainali kwetu, ushindi ni muhimu kuliko chochote na ninalijua hilo hivyo tunaomba mashabiki zetu waje kwa wingi kutuunga mkono," amesema.

Tags: