Nyota 3 Yanga waongeza nguvu kuivaa Mashujaa FC

Nahodha wa timu ya Yanga, Bakari Nondo

KANDANDA Nyota 3 Yanga waongeza nguvu kuivaa Mashujaa FC

Zahoro Juma • 05:30 - 08.02.2024

Wachezaji hao walikosekana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kucheza michuano ya AFCON

Wakati kikosi cha timu ya Yanga SC, kikijiandaa kushuka uwanjani kesho kuumana na Mashujaa FC, nyota watatu wa timu hiyo wameongeza nguvu baada ya kukosekana katika mechi mbili zilizopita.

Nyota hao ni nahodha, Bakari Nondo, Augustine Okrah na Ibrahim Abdullah 'Bacca' ambao wote walikosa mechi dhidi ya Kagera Sugar na Dodoma Jiji kutokana na sababu mbalimbali.

Nondo na Bacca walipewa mapumziko baada ya kuiwakilisha Tanzania 'Taifa Stars' katika michuano ya AFCON inayoendelea nchini Ivory Coast.

Wakati Okrah alikuwa amepewa programu maalum ya kurudisha utimamu wa mwili baada ya kuumia wakati wa michuano ya Mapinduzi Cup.

Wachezaji hao wanatarajia kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga baaada ya kushiriki mazoezi ya timu yaliyofanyika jana na leo jijini Dar es Salaam.

Yanga itacheza mchezo huo kesho saa 1 usiku Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni mara yao ya pili mfululizo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi iliyopita.

Hata hivyo, Kocha Miguel Gamondi bado atalazimika kuendelea kukosa huduma ya wachezaji wake wawili nyota kwenye kikosi cha kwanza Stephan Aziz Ki na Djigui Diarra ambao wamechelewa kurudi nchini baada ya ushiriki wao katika michuano ya Afcon.

Kocha Gamondi akizungumza kuelekea mchezo huo, amesema anajua umuhimu mkubwa wa alama tatu katika michezo ambayo inaendelea hivi sasa kwasababu ushindani katika ligi msimu huu ni mkubwa.

"Msimu huu ushindani ni mkubwa, kila timu inajiandaa kufanya vizuri hivyo hatupaswi kupoteza alama mara kwa mara," amesema Gamondi.

Kwa upande wa Kocha wa Mashujaa FC, Mohamed Baresi, amesema ukubwa wa Yanga hauwafanyi wao kuogopa kukabiliana nao uwanjani.

Katika hatua nyingine, Klabu ya Yanga, imerudisha shughuli zote za kiofisi katika majengo yao ya makao makuu na sio katika Jengo la Salamander ambalo wamekuwa wakilitumia kwa miaka ya hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said wakati wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa ofisi hizo ambazo zimekamilika kufanyiwa ukarabati mkubwa.