Simba SC yaipiga 4G Tabora United Ligi Kuu

Straika mpya wa Simba, Freddy Koublan, akishangilia bao lake

KANDANDA Simba SC yaipiga 4G Tabora United Ligi Kuu

Zahoro Juma • 20:30 - 06.02.2024

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa timu hiyo na kuifanya ijikite katika nafasi ya tatu ikiwa na alama 29 ikitanguliwa na Azam FC na Yanga SC

Washambuliaji wapya wa timu ya Simba SC, Freddy Koublan na Pa Omar Jobe, kila mmoja amefunga bao moja na kuisaidia timu yao kuibuka na ushindi mnono wa ugenini wa mabao 4-0 dhidi ya Tabora United.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, ulikuwa moja kati ya mechi ambazo zimepata wahudhuriaji wengi uwanjani msimu huu.

Huo unakuwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa Simba ambao walitoka Kigoma siku mbili zilizopita kuvuna alama tatu mbele ya Mashujaa.

Mshambuliaji Pa Omar Jobe raia wa Gambia ndiye alikuwa wa kwanza kufungua kurasa ya mabao kwa kuandika bao la utangulizi dakika ya 19 baada ya kuunganisha krosi ya kiungo, Clotus Chama ambaye alianza katika mchezo huu kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza sakata lake.

Hili linakuwa ni bao la kwanza kwa Jobe kwenye Ligi Kuu Bara lakini ni la pili katika michuano yote ukijumlisha na lile alilofunga kwenye mechi ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Tembo.

Simba waliendelea kulisakama lango la Tabora United na dakika ya 36 walifunga bao la pili safari hii akiwa ni kiungo raia wa Mali, Sadio Kanoute aliyefunga kwa kichwa akitumia vyema krosi kutoka kwa Shomari Kapombe.

Mbali na mabao hayo lakini pia Simba ndani ya kipindi cha kwanza walikosa nafasi za kufunga mabao kupitia kwa Chama na Saido Ntibanzokiza ambaye mpira wake alioupiga akiwa nje ya boksi uligonga mwamba.

Dakika ya 66, mlinzi wa Simba, Che Fondoh Malone, alifunga bao la tatu na ikiwa ni la kwanza kwake akiwa na timu hiyo akimalizia pasi ya Chama baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Tabora United.

Karamu ya mabao kwa Simba ilitamatishwa na Koublan ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukuwa nafasi ya Jobe na yeye akaandika bao lake la kwanza baada ya kucheza mechi mbili za ligi tangu asajiliwe.

Majaribio yao yote yakutaka kuliandama lango la Simba yalizimwa vyema katikati ya uwanja na safu ya kiungo iliyokuwa chini ya Babacar Sarr.

Simba sasa wamefikisha alama 29 wakijikita zaidi katika nafasi ya tatu na wakiendelea kuwapa presha vinara waliokuwa juu yake Azam FC na Yanga SC.

Kwa upande wa Tabora United, wao wataendelea kusalia katika nafasi yao ya 13 wakiwa na alama zao 15 baada ya kushuka dimbani mara 14.