Straika mpya Yanga SC afunguka kufunga mabao mawili

KANDANDA Straika mpya Yanga SC afunguka kufunga mabao mawili

Na Zahoro Juma • 08:30 - 22.02.2024

Nyota huyo ni Joseph Guede ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo na kucheza mechi tano mfululizo bila kuona nyavu

Straika mwili nyumba wa timu ya Yanga SC, Joseph Guede, amesema mabao mawili aliyofunga kwenye mchezo wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Polisi Tanzania ni mwanzo tu na watu watarajie makubwa zaidi.

Ameongeza kwa kusema anashukuru amefunga mabao hayo kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afria dhidi ya CR Belouizdad, hivyo anaamini yatamuongezea hali ya kujiamini.

"Huu ni mwanzo tu lakini naamini nitaendelea kufanya vizuri, ninachojivunia ni kwamba nimefunga ikiwa tupo katika maandalizi ya kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa na hii itaniongezea hali ya kujiamini," amesema Guede baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa jana uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na Yanga kushinda mabao 5-0.

Guede alisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili akitokea nchini Uturuki lakini katika mechi nne za ligi alizocheza alikuwa hajafunga bao lolote kitu ambacho kilianza kuzusha hofu miongoni mwa mashabiki wa soka nchini.

Katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania, mbali na Guede wachezaji wengine waliofunga ni Farid Mussa, Shekhan Ibrahim na Clement Mzize.

Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema alimwambia Guede akafunge katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania lakini alimtahadharisha kuwa apunguze presha.

"Kuelekea mchezo huu nilimwambia Guede leo inabidi ufunge lakini tafadhali usiwe na presha," amesema Gamondi.

Kuelekea mechi ya Jumamosi dhidi ya Belouizdad, Gamondi amesema bado wanaendelea na maandalizi na wanaamini wanaweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo.

Yanga katika mchezo huo, walipumzisha wachezaji takribani tisa wa kikosi cha kwanza ambao hawakuwa hata sehemu ya kukaa benchi.

Wakati huo huo, kikosi cha CR Belouizdad kutoka Algeria, tayari kimeshatua nchini leo mchana na sasa wanafanya maandalizi yao kuelekea mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Yanga na Belouizdad zote zina alama 5 katika msimamo wa Kundi D ambapo mechi baina yao inaweza kuwa na taswira kubwa ya kuamua timu ya kwenda hatua ya robo fainali kabla ya mechi za mwisho ambazo zinatarajia kuchezwa mwanzo wa mwezi ujao.

Tags: