Simba SC yapania kuvunja rekodi ya Asec Mimosa

Straika mpya wa Simba SC, Fredy Kouablan, akiwa tayari kwa safari

KANDANDA Simba SC yapania kuvunja rekodi ya Asec Mimosa

Na Zahoro Juma • 22:14 - 20.02.2024

Ni katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utachezwa Ijumaa huku Asec ikiwa haijapoteza mechi yoyote ya Kundi B

Timu ya Simba SC, imeondoka nchini leo kwenda Ivory Coast ambapo wamepania kwenda kuvunja rekodi ya Asec Mimosa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajia kuchezwa Ijumaa.

Asec ambao ni vinara wa Kundi B, ikiwa na alama 10 na tayari ikiwa imeshafuzu hatua ya robo fainali lakini pia wanashikilia rekodi ya kutopoteza mchezo wowote hadi sasa kwenye kundi lao.

Akizungumza wakati akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema Asec ni wapinzani wazuri na wanatarajia mchezo wa ushindani lakini wao wamejipanga kwa ajili ya kwenda kushinda.

"Tunajua tunakabiliana na mpinzani ambaye ni mgumu haswa, hata hivyo maandalizi yetu yalijikita kwa ajili ya kwenda kufanya vizuri katika mchezo huu ambao tunakwenda kuucheza Ijumaa," amesema.

Matola aliongeza wanasikitika kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo adhabu ya kadi za njano lakini jambo jema pia wamewapokea wachezaji wengine kikosini akiwemo Henock Inonga.

Simba na Asec walicheza mechi ya kwanza Novemba, mwaka jana ambapo matokeo ya wawili hao ilikuwa ni sare ya kufungana bao 1-1.

Kumbukumbu ya mwisho ya Simba kucheza na Asec ugenini, ilikubali kichapo cha mabao 3-0 lakini mechi hiyo ilichezwa nchini Gambia.

Simba inahitaji ushindi au matokeo hata ya sare ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele hasa pale watakaporudi Dar es Salaam kwa ajili ya kucheza mechi yao ya mwisho nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Katika safari ya kwenda Ivory Coast, mbali na kipa Ayoub Lakred ambaye amebaki nchini kutokana na kadi tatu za njano lakini pia Willy Onana hajasafiri kutokana na majeraha ya nyama za paja ambayo alipata tangu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Wachezaji vijana ambao wamesajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la usajili, Edwin Balua, Ladack Chasambi na Saleh Karabaka pia hawakuwa sehemu ya safari hiyo ikielezwa kuwa hawapo katika mipango ya kocha katika mchezo huo.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, mlinzi wa pembeni, David Kameta 'Duchu', amesema wamefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo na aliwaomba mashabiki wao wasiwe na wasiwasi juu ya kikosi chao.

Tags: