Yanga SC yapania kulipa kisasi kwa CR Belouizdad

Uganda Cranes midfielder Khalid Aucho during training with Young Africans | Image by Young Africans

KANDANDA Yanga SC yapania kulipa kisasi kwa CR Belouizdad

Na Zahoro Juma • 18:32 - 19.02.2024

Yaupa jina la Pacome Day mchezo huo ambao utapigwa Jumamosi Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam

Klabu ya Yanga SC, imetangaza vita ya kutaka kulipa kisasi dhidi ya CR Belouizdad kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajia kuchezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Algeria, Yanga ilikubali kichapo cha mabao 3-0.

Timu hizo zote kwa sasa zimecheza michezo minne na kila mmoja akiwa na alama tano lakini Belouizdad wapo nafasi ya pili nyuma ya Al Ahly kutokana na faida ya mabao dhidi ya Yanga ambao wametulia nafasi ya tatu.

Kuelekea mchezo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe ametangaza mchezo huo utakwenda kwa jina la 'Pacome Day' ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao ambao wameufanya katika michezo yao kadhaa ya nyumbani ya michuano hiyo.

"Mchezo huu ni muhimu kwetu kama kweli tunataka kuvuka kwenda robo fainali, kutokana na umuhimu huo tumeupa jina la Pacome Day ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha," amesema.

Pacome amekuwa ni moja kati ya nguzo muhimu kwa Yanga katika michuano hiyo akifunga bao moja kwenye kila mchezo katika michezo mitatu ya mwisho na kuwa mmoja kati ya vinara wa upachikaji mabao msimu huu akiwa na mabao matatu nyuma ya kinara Sankara Karamoko wa Asec Mimosa mwenye mabao manne.

Yanga wanalazimika kusaka ushindi katika mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele kwenda hatua ya robo fainali ambayo pia itakuwa ni rekodi katika historia ya timu yao.

Kamwe amesema mchezo huo utapigwa saa 1 usiku na wageni wao, Belouizdad wanatarajia kutua nchini kesho.

Mara ya mwisho Yanga kucheza mechi katika mashindano hayo ilikuwa ni Desemba 20, mwaka jana ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Medeama kutoka nchini Ghana.

Kwa mujibu wa Kamwe, kikosi kwasasa kipo kambini tangu kiliporejea kutoka Morogoro kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC na maandalizi kuelekea mchezo wa Belouizdad yameanza chini ya Kocha, Miguel Gamondi.

Katika hatua nyingine, timu hiyo, leo saa 1 usiku inatarajia kushuka Uwanja wa Azam Complex kucheza mechi ya Azam Sports Federration Cup (ASFC) dhidi ya Polisi Tanzania.

Mchezo huo wa hatua ya 32 Bora utakuwa ni mwendelezo wa michezo mingine ambayo ilianza kuchezwa tangu jana.