Fei Toto amkimbiza Aziz KI kwa mabao Ligi Kuu

KANDANDA Fei Toto amkimbiza Aziz KI kwa mabao Ligi Kuu

Zahoro Mlanzi • 12:31 - 22.12.2023

Kiungo huyo wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' na Azam FC, bado bao moja kumfikia kinara wa mabao, Stephane Azizi KI wa Yanga

Kiungo Mshambuliaji wa timu ya Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', ameendelea kumkimbiza kimabao mchezaji wa Yanga SC, Stephane Azizi KI ambapo sasa bado bao moja amfikie.

Fei Toto amefunga bao mojawapo katika ushindi walioupata timu yake wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar ugenini, mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Hilo ni bao lake la 8 msimu huu kwa kiungo huyo tangu alipojiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Yanga SC huku Azizi KI akiongoza kwa mabao yake 9.

Wengine wanaofuata kwa karibu katika upachikaji mabao ni Maxi Nzengeli wa Yanga na Jean Baleke wa Simba wenye mabao 7 kila mmoja.

Mabao mengine ya Azam katika mchezo huo uliowafanya wafikishe alama 31, yalifungwa na Mzimbabwe Prince Dube, Pascal Msindo na Msenegal, Allasane Diao.

Huo ni ushindi wa sita mfululizo kwa Azam tangu ilipofungwa mara ya mwisho mabao 3-0 na Namungo FC.

Pamoja na Azam kujikusanyia alama hizo, miamba ya soka la Tanzania, timu za Yanga na Simba zipo nyuma kwa michezo mitatu na minne tofauti tofauti.

Miamba hiyo itashuka uwanjani ugenini kesho ambapo Yanga itaumana na Tabora United mkoani Tabora na Simba itakuwa na kazi kwa Mashujaa FC mkoani Kigoma.

Fei Toto ndiye aliyekuwa wa kwanza kufungua kalamu ya mabao hayo, akifunga katika dakika ya 9 ya mchezo na kuwapa wakati mgumu Kagera Sugar.

Hata hivyo, katika mchezo huo, Kipa mzawa, Zuberi Foba, aliokoa mkwaju wa penalti wa mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 49.

Kwa upande wa Kagera Sugar, hicho ni kipigio cha nne mfululuzo katika ligi hiyo na inabaki na pointi zake 13 kutokana na kucheza mechi 13 ikiwa nafasi ya 14 kwenye ligi ya timu 16.

Tags: