Tabora United yamtambulisha straika mpya wa Kinigeria

KANDANDA Tabora United yamtambulisha straika mpya wa Kinigeria

Zahoro Juma • 16:00 - 29.01.2024

Timu hiyo ambayo imepanda daraja, inapambana kubaki katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara

Uongozi wa timu ya Tabora United, umeweka wazi unajivunia ujio wa nyota wao mpya, Emotan Cletus Eba, baada ya kuwasili leo nchini Tanzania kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo.

Tabora United ni miongoni mwa timu ambazo zimepanda daraja zikiwa zinapambana kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Tabora United, Chritina Mwagala, wachezaji wao wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuwa kwenye ubora kitaifa na baadaye kimataifa.

“Emotan Cletus Eba, ni fundi halisi wa mpira kutoka Nigeria, ametua Tabora United,” amesema Mwagala.

Amesema Eba, 23 ametokea timu ya Sunshine Stars inayoshiriki Ligi Kuu Nigeria ambapo amezaliwa mjini Ekong na amekuwa na uwezo mzuri wa kufunga na kutoa asisti ya mabao.

Pia Eba aliwahi kucheza katika timu ya Rivers United ambapo alicheza michezo mbalimbali ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Tabora United inashika nafasi ya 12 ikiwa na alama 15 baada ya kucheza michezo 13, ikishinda mitatu, sare sita na kufungwa minne.

Tags: