Nahodha Singida FG atimkia Cape Town City ya Afrika Kusini

Nahodha wa Singida FG, Gadiel Michael, akizungumzia usajili wake

KANDANDA Nahodha Singida FG atimkia Cape Town City ya Afrika Kusini

Festus Chuma • Na Zahoro Juma • 18:37 - 17.01.2024

Mchezaji huyo ni Mtanzania Gadiel Michael ambaye aliwahi kuzichezea Azam, Yanga na Simba kwa nyakati tofauti

Nahodha wa timu ya Singida FG, Gadiel Michael, amesajiliwa na timu ya Cape Town Spurs inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Afrika Kusini.

Hayo amethibitisha Rais wa timu hiyo, Japhet Makau wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Gadiel ambaye aliwahi kucheza Azam na Yanga alijiunga na Singida FG mwanzo wa msimu uliopita akitokea Klabu ya Simba ambayo alidumu nayo kwa kipindi cha miaka minne.

Mlinzi huyo wa kushoto alikuwa ni sehemu ya kikosi cha Singida FG kilichoshiriki Kombe la Mapinduzi, Zanzibar kabla ya kuondoshwa na Simba katika hatua ya nusu fainali.

Timu anayojiunga nayo inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi ya Afrika Kusini wakiwa wamekusanya alama 4 katika michezo 16 ambayo wameshuka dimbani msimu huu.

Katika mkutano huo, pia Makau amegusia kuhusu tetesi za Singida FG kupitia kipindi kigumu cha ukata wa fedha.

Makau amesema adhabu mfululizo walizopata kutoka FIFA zimewayumbisha kiuchumi hivyo kama timu walikuja na mkakati wa kukusanya vyanzo kutoka katika vyanzo vyao ikiwemo kuuza baadhi ya wachezaji ambao wana soko.

Amesema mbali na Gadiel lakini pia waliwauza baadhi ya wachezaji wengine ndani na nje ya nchi ambao hakuwa tayari kuwataja.

Katika dirisha hili la usajili Singida FG, haikutangaza kusajili mchezaji yeyote bali wachezaji wake wengi nyota wamekuwa wakihusishwa na kuihama timu hiyo.

Mbali na Gadiel lakini pia mshambuliaji, Meddie Kagere, alitangazwa kuhamia timu ya Namungo ya mkoani Lindi siku ya mwisho ya usajili.