Singida FG yautaka ubingwa wa Mapinduzi Cup

KANDANDA Singida FG yautaka ubingwa wa Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 20:13 - 26.12.2023

Bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu ataondoka na sh. milioni 100 za Kitanzania

Baada ya kulikosa taji la Mapinduzi Cup msimu uliopita, uongozi wa Klabu ya Singida FG, umedhamiria kufanya kweli msimu huu kwa kuamua kubeba jeshi la wachezaji wote wa kikosi cha kwanza kwenda kushiriki michuano hiyo msimu huu.

Kikosi cha Singida kipo katika maandalizi ya mwisho kabla ya kuingia Zanzibar ambapo watacheza mchezo wao wa kwanza Desemba 29 dhidi ya timu ya Jamhuri.

Akizungumza na Pulsesports, Ofisa Habari wa timu ya Singida, Hussein Masanza, amesema msimu huu wamepania kufanya vizuri kuliko msimu uliopita ambapo wanataka kutwaa ubingwa.

"Msimu uliopita ilikuwa ni mara yetu ya kwanza kushiriki lakini tukafikia hatua ya fainali, msimu huu hatuhitaji kurudia makosa tuliyofanya msimu uliopita," amesema.

Msimu uliopita Singida walikwama kwenye mchezo wa fainali ambapo walifungwa 2-0 na Mlandege ambao kwasasa ndio mabingwa watetezi.

Mashindano ya mwaka huu kwa kiasi kikubwa yameboreshwa kwani bingwa ataondoka na sh. milioni 100 badala ya sh. milioni 50 za mwaka jana na mshindi wa pili atapata sh. milioni 70.

Pia viingilio kwa ajili ya mashindano hayo, vimeweka wazi ambapo katika hatua ya awali, mechi za jioni ni sh. 5,000 na sh. 3,000, mechi za usiku ni sh. 10, 000, sh. 5,000, sh. 3,000 huku sh. 100,000 kwa VIP mechi zote.

Nusu fainali zitapigwa katika viwanja wiwili tofauti moja itachezwa Uwanja wa Amaan Unguja na nyingine Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Tags: