Azam FC yaongeza ugumu mbio za ubingwa

KANDANDA Azam FC yaongeza ugumu mbio za ubingwa

Na Zahoro Juma • 11:00 - 17.02.2024

Ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold

Bao la ushindi la winga, Idd Nado, limeipa ushindi wa mabao 2-1 na alama tatu timu ya Azam FC ambayo ilikuwa inacheza na Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo wa kufunga duru ya kwanza kwa timu zote mbili, ulichezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Geita ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa mshambuliaji wao, Tariq Seif dakika ya 41 lakini bao hilo lilidumu kwa dakika tatu kabla ya Gibril Sillah kusawazisha.

Nado alifunga bao la ushindi dakika ya 81 ya mchezo baada ya walinzi wa Geita kumuacha akiwa peke yake ndani ya eneo la boksi.

Ushindi huo, umezidi kuchochea vita ya timu tatu za juu ambapo sasa Azam amefikisha alama 35 ikiwa ni alama moja nyuma ya Simba kwenye nafasi ya pili.

Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na alama zao 40 na tayari timu zote zimecheza mechi 15 za mzunguko wa kwanza.