Kocha Taifa Stars kuifungia kazi DR Congo mechi ya mwisho

KANDANDA Kocha Taifa Stars kuifungia kazi DR Congo mechi ya mwisho

Zahoro Juma • 20:11 - 22.01.2024

Mchezo huo utakuwa wa Kundi F linaloongozwa na Morocoo yenye alama 4 huku kila timu ikionekana kuwa na nafasi ya kutinga 16 Bora

Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Hemed Seleman 'Morocco', amesema njia yao ya kupita kwenda 16 Bora ya michuano ya Afcon ipo kwenye mechi yao ya mwisho ambayo watacheza na DR Congo.

Stars kwasasa wanaburuza mkia kwenye Kundi F wakiwa na alama 1 baada ya kushuka uwanjani mara mbili kucheza dhidi ya Morocco na Zambia.

Katika mechi iliyopita dhidi ya Zambia, Tanzania ilipoteza nafasi ya kuweka rekodi ya kushinda mchezo wao wa kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kuruhusu bao la jioni lililosababisha matokeo ya sare ya bao 1-1.

Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa winga wao, Simon Msuva aliyefunga kwenye kipindi cha kwanza lakini licha ya kuwa Zambia walikuwa pungufu kwa muda mwingi wa mchezo walijikuta wakisawazisha bao kwenye dakika ya 88 ya mchezo kupitia kwa Patson Daka.

Matokeo hayo ya sare ambayo yaliwaumiza Watanzania wengi, yamewafanya Stars kuendelea kuburuza mkia kwenye kundi hilo wakiwa na alama yao moja huku Morocco wakiwa ni vinara na alama 4 wakati Zambia na DR Congo wote wakiwa na alama 2.

Ili kufuzu Stars inahitajika kupata ushindi dhidi ya DR Congo katika mchezo wa mwisho ambao utachezwa Januari 24 huku pia wakiomba Zambia asiweze kushinda wakati wanacheza na Morocco siku hiyo.

"Kikosi chetu kimeimarika ukilinganisha na jinsi tulivyoanza michuano, timu imeonesha mabadiliko ya kiuchezaji na tunaamini mchezo wa mwisho tutabadilika zaidi," amesema Morocco.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kushiriki michuano ya Afcon. Mara ya kwanza walishiriki mwaka 1980 nchini Nigeria ambapo walijikuta wakipoteza michezo miwili mbele ya wenyeweji Nigeria na kisha Misri kabla ya kwenda sare ya 1-1 na Ivory Coast.

Stars ilifuzu tena kushiriki Afcon mwaka 2019 nchini Misri ambapo katika michezo yake mitatu ya Kundi C ilijikuta ikipoteza mbele ya Algeria, Senegal na Kenya.