Chama aiokoa Simba kufungwa ugenini na Power Dynamos

© Kwa Hisani

KANDANDA Chama aiokoa Simba kufungwa ugenini na Power Dynamos

Zahoro Mlanzi • 20:36 - 16.09.2023

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, umepigwa uwanjani Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.

Mabao mawili yaliyofungwa na kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama, yameikoa timu yake ya Simba SC kufungwa ugenini baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Power Dynamos.

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, umepigwa uwanjani Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.

Katika mchezo huo ambao haukuwa na mashabiki wengi kabisa licha ya Simba kwenda na mashabiki wao katika mabasi matatu kutoka Dar es Salaam, ulikuwa na ushindani mkubwa tofauti na ilivyodhaniwa na mashabiki wengi wa Simba.

Bao la kwanza la Dynamos, limetokana na kujifunga kwa beki wa Simba, Mkongo Henock Inonga ambaye akiwa katika jitihada wa kuokoa mpira uliopigwa na Joshua Mutale dakika ya 28 akajikuta akiutumbukiza wavuni huku Kipa, Ayoub Lekred raia wa Morocco akiwa Hans la kufanya.

Baada ya kufungwa bao hilo, Simba imesawazisha kupitia kwa Chama dakika ya 62 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na Kipa, Lawrence Mulenga kutokana na shuti la Muzamir Yassin na kukwamisha wavuni.

Wakiwa bado wana furaha ya kufunga bao la ugenini, dakika ya 74, Cephas Mulombwa amepiga shuti nje ya eneo la hatari lililotinga moja kwa moja wavuni huku Lakred akijitahidi kupangua na kumzidi nguvu.

Dynamos ikiwa na matumaini ya kuanza na ushindi katika mchezo huo wa nyumbani, zikiwa zimeongezwa dakika 6, Chama akiwa nje kidgo ya eneo la hatari amepiga shuti kwa mguu wa kushoto na kujaa moja kwa moja wavuni.

Timu hizo zitarudiana Jijini Dar es Salaam Jumapili ijayo na mshindi wa jumla atakwenda hatua ya 16 Bora ambayo itachezwa kwa mfumo wa makundi.