Yanga yaenda Kigali bila nahodha Mwamnyeto

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga yaenda Kigali bila nahodha Mwamnyeto

Zahoro Mlanzi • 14:00 - 15.09.2023

Yanga itashuka uwanjani Pele mjini Kigali, Jumamosi saa 10 jioni kuumana na timu hiyo katika mechi ya mkondo wa kwanza wa michuano hiyo.

Kikosi cha wachezaji 26 wa timu ya Yanga, kimeondoka nchini muda si mrefu kwenda Rwanda kwa ajili ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Merreikh ya Sudan bila nahodha wao, Bakari Mwamnyeto.

Mwamnyeto ameshindwa kuondoka na wenzake baada ya kupata changamoto ya masuala ya kifamilia nyumbani kwao jijini Tanga.

Yanga itashuka uwanjani Pele mjini Kigali, Jumamosi saa 10 jioni kuumana na timu hiyo katika mechi ya mkondo wa kwanza wa michuano hiyo.

Wakati kikosi hicho kikiondoka kwa ndege, tayari mabasi zaidi ya 50 yalianza safari alfajiri ya leo kwenda nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mtandao wa kijamii wa klabu hiyo, iliwataja wachezaji wote waliosajiliwa msimu huu kuwemo katika safari hiyo isipokuwa Mwamnyeto.

Hata hivyo, Kocha Muargentina, Miguel Gamondi ameridhia Mwamnyeto kutokuwa sehemu ya kikosi kinachokwenda mjini Kigali kwa ajili ya mchezo huo.

Akizungumza kabla ya kuanza safari, Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison, amesema wachezaji wote wana morali ya juu kuelekea mchezo huo.

"Hatuna mchezaji ambaye majeruhi, wote wapo imara na ukizingatia wamepata motisha kutoka kwa mashabiki na wanachama wetu ambao walianza safari tangu asubuhi," amesema Harrison.

Amesema mchezaji pekee ambaye hatokwenda ni nahodha Mwamnyeto yeye ana udhuru wa kwenda kushughulikia masuala ya kifamilia.

Wachezaji walioondoka ni makipa Djugui Diarra, Metacha Mnata na Abutwalib Mshery, mabeki ni Dickson Job, Ibrahim Abdullah, Gift Fred, Kibwana Shomari, Lomalisa Mutambala, Nickson Kibabage na Kouassi Yao.

Viungo ni Khalid Aucho, Jonas Mkude, Zawadi Mauya, Mudathir Yahya, Salum Abubakari, Farid Mussa, Crispin Ngushi, Jesus Moloko, Denis Nkane na Mahlatse Makudubela 'Skudu'.

Wakati washambuliaji ni Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Stephen Aziz KI, Clement Mzize, Kennedy Musonda na Hafiz Konkoni.