Yanga yaitandika Al Merreikh 2-0, yanusa hatua ya makundi Afrika

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga yaitandika Al Merreikh 2-0, yanusa hatua ya makundi Afrika

Zahoro Mlanzi • 19:40 - 16.09.2023

Timu hizo zitarudiana tena mwishoni mwa mwezi huu uwanjani Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Timu ya Yanga SC, imeanza vizuri mechi yake ya ugenini dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Pele jijini Kigali, Rwanda.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, yalifungwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize.

Yanga ambao walionekana kama wapo nyumbani kutokana na uwanja wote kutawaliwa na mashabiki wao waliosafiri kwa mabasi zaidi ya 50 kushangilia muda wote wa mchezo, timu hizo zikaenda mapumziko zikishindwa kufungana.

Lakini imewachukua dakika 15 tangu kuanza kwa kipindi cha pili, Yanga kufunga bao la kwanza kupitia kwa mtokea benchi, Musonda kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Pacome Zoazoua.

Musonda ambaye ameingia badala ya Mudathir Yahya, amewazidi ujanja mabeki wa Marreikh na kuruka juu na kuugonga mpira uliokwenda kujaa wavuni huku Kipa, Mohamed Almustapha akiruka bila mafanikio.

Kufungwa kwa bao hilo, limeifanya Yanga kuongeza kasi katika kushambulia lakini Merreikh wameendelea kucheza soka lao la utulivu na kupiga pasi fupi fupi kwenda mbele.

Wakati wachezaji wa Merreikh wakionekana kama wanatafuta njia ya kuivuka safu ya ulinzi ya Yanga, ndipo wakafanyiwa shambulizi la kushtukiza lililozaa bao la pili kwa Yanga.

Straika kinda wa Kitanzania, Mzize ameifungia Yanga bao la pili akiwa ndani ya eneo la hatari kwa kupiga shuti lililoshindwa kudakwa na Kipa Almustapha na mpira kujaa wavuni, akipokea pasi ya kisigino ya Stephano Azizi KI.

Katika mchezo huo, Merreikh haikufanikiwa kupiga shuti lililolenga goli zaidi ya mashuti yote waliyopiga yalipaa juu ya goli.

Timu hizo zitarudiana tena mwishoni mwa mwezi huu uwanjani Azam Complex jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atakuwa ametinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.