Azam FC yaingia hofu michuano ya Mapinduzi Cup

KANDANDA Azam FC yaingia hofu michuano ya Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 21:13 - 27.12.2023

Hali hiyo inatokana na kudai kuwa kwa sasa timu hiyo ipo katika kiwango bora, hivyo timu nyingi itacheza kwa nguvu ikikutana nayo

Wakati timu ya Azam FC, ikitarajia kuanza kusaka taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi kesho, uongozi wa timu hiyo umedai wanahofia kukamiwa kutokana na kiwango chao bora msimu huu.

Akizungumza wakati wakiwa bandarini kwenda visiwani Zanzibar, Ofisa Habari wa timu hiyo, Hashim Ibwe, amesema wamelenga kufanya vizuri kwenye michuano hiyo msimu huu na ndio maana wameondoka na nyota wao wengi wa kikosi cha kwanza.

Amesema wamesafiri na nyota 25 ambapo 18 kati yao ni wachezaji wa kikosi cha kwanza na 7 ni nyota kutoka katika timu zao za vijana.

Hata hivyo amebainisha kutokana na ubora ambao wamekuwa nao msimu huu kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara wanaona kuwa timu nyingi zitawakamia hivyo wamejiandaa kwa ajili ya kwenda kushindana.

"Unajua timu yetu kwasasa ina ubora mkubwa, hii si habari nzuri kwa timu nyingine hasa zinazoshiriki Mapinduzi Cup na badala yake kuna uwezekano wa kukamiwa katika mechi zetu," amesema.

Azam wanakwenda kushiriki michuano hiyo katika kipindi hiki cha mapumziko huku wakiwa ni vinara wa ligi hiyo ya bara hadi sasa ambapo wana alama 31 baada ya kushuka dimbani mara 13.

Katika michuano ya Mapinduzi Cup, wamewekwa Kundi A sambamba na timu za Mlandege FC, Vital'O na Chipukizi United.

Tags: