Al-Merreikh, Yanga kuchezea Rwanda michuano ya CAF

© Yanga

KANDANDA Al-Merreikh, Yanga kuchezea Rwanda michuano ya CAF

Zahoro Mlanzi • 19:00 - 02.09.2023

Hatua hiyo imekuja baada ya sintofahamu iliyoibuka kwa kuelezwa mchezo huo ungepigwa nchini Tunisia.

Hatimaye timu ya Al-Merreikh ya Sudan, imeamua mchezo wake wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga sasa uchezewe nchini Rwanda.

Hatua hiyo imekuja baada ya sintofahamu iliyoibuka kwa kuelezwa mchezo huo ungepigwa nchini Tunisia.

Michezo ya kimataifa inashindwa kuchezewa nchini Sudan kutokana na usalama kuwa mdogo unaosababishwa na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Klabu ya Yanga kupitia Ofisa Habari wao, Ally Kamwe, mchezo huo utapigwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Pele jijini Kigali nchini humo.

Ofisa huyo aliwataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuanza maandalizi mapema ya safari ili kwenda kuwapa sapoti wachezaji wao.

"Mchezo wetu wa mkondo wa kwanza raundi ya kwanza dhidi ya Al-Merreikh utapigwa Septemba 16 jijini Kigali, Rwanda, hivyo mashabiki tunahitaji sapoti yenu katika mchezo huu wa ugenini," alisema Kamwe.

Alisema malengo yao ni kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo na watapambana kufikia hatua hiyo.

Msimu uliopita Yanga ikicheza fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ila ikafungwa na USM Algers ya Algeria.

Yanga ilianzia raundi ya awali katika michuano hiyo na kuiondoa ASAS FC ya Djibouti kwa jumla ya mabao 9-1 huku Merreikh ikiitoa AS Otoho ya Congo Brazzaville baada ya mchezo wa awali kutoka suluhu na ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.