Simba SC yataja malengo mawili ya msimu wa 2023/24 baada ya kutoka mkono mtupu msimu uliopita

FOOTBALL Simba SC yataja malengo mawili ya msimu wa 2023/24 baada ya kutoka mkono mtupu msimu uliopita

Zahoro Mlanzi • 16:49 - 01.09.2023

Katika misimu miwili iliyopita, klabu hiyo imeshindwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Klabu ya Simba SC, imeweka wazi msimu huu 2023/24 malengo yao ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika misimu miwili iliyopita, klabu hiyo imeshindwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara badala yake watani zao wa jadi, timu ya Yanga ndio iliyotwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo.

Kwa upande wa michuano ya kimataifa, timu hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa miaka minne mfululizo ikicheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza Dar es Salaam kuelekea mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia utakaopigwa Septemba 16, Ofisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wamekosa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara misimu miwili mfululizo, lakini msimu huu wamejipanga kurudisha heshima yao.

"Wana-Simba msiwe na hofu, msimu huu tumejipanga vizuri kuhakikisha tunarudisha heshima yetu...ndio maana tuliweka kambi ya siku 21 nchini Uturuki huku tukiwa tumefanya usajili wa wachezaji nyota kutoka maeneo mbalimbali barani Afrika," alisema Ally.

Alisema silaha zao za ushindi kwenye mechi za kimataifa lazima ziandaliwe vizuri na wanajua ili kupata ushindi lazima wachezaji wawe tayari na hilo wanalitambua.

“Kila kitu tunaamini kitakuwa sawa wapinzani wetu (Dynamos) tunatambua wanajua wanakutana na timu ya aina gani. Inapofikia hatua ya mechi za kimataifa hilo ni suala kubwa na tunawaheshimu wapinzani wetu ila ambacho tunafanya ni kuwa tayari,” alisisitiza Ally.

Alisema kwa sasa wana mpango wa kuweka kambi nje ya nchi na ikishindikana wataweka hapa hapa nchini.

Aliongeza kipindi hicho watakachokuwa kambini watacheza mechi mbili za kirafiki ili wawe fiti kukabiliana na Dynamos.

Hivi sasa Ligi ya Tanzania Bara imesimama kupisha mechi za kimataifa kuwania kufuzu AFCON 2024 zitakazofanyikia nchini Ivory Coast.

Tags: