Yanga SC yaingia kambini kujiandaa na Mtibwa Sugar

LIGI KUU Yanga SC yaingia kambini kujiandaa na Mtibwa Sugar

Zahoro Mlanzi • 20:12 - 11.12.2023

Itaingia katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya pili kwa alama 24 nyuma ya Azam FC ambayo inaongoza kwa alama 25 lakini ipo mbele kwa michezo miwili

Baada ya kurejea nchini Jumapili wakitokea Ghana, wachezaji wa timu ya Yanga SC, leo wameingia rasmi kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuziwinda alama tatu za mchezo wa Ligi Kuu Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Jumamosi.

Mchezo huo utakuwa ni wa 10 kwa Yanga ambao hadi sasa wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama zao 24.

Wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko ya muda mfupi baada ya kutoka nchini Ghana ambapo Ijumaa walicheza mechi ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Medeama SC na kuvuna alama moja baada ya kutoka sare ya 1-1.

Mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, utakuwa ni kwanza kwa Yanga tangu waliposhuka dimbani mara ya mwisho Novemba 8 ambapo walicheza Mkwakwani na kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union.

Wanakutana na Mtibwa Sugar ambao kwasasa wapo kati hali mbaya wakiwa na alama 5 mkiani huku wakiwa wameshuka dimbani mara 13.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema timu ilipata mapumziko kama ilivyo kawaida kwasababu wametoka katika mchezo mgumu wa nje ya nchi lakini sasa wanarejea kazini katika mechi za ligi kuu.

"Tulikuwa na mapumziko ya wachezaji na benchi la ufundi lakini kwa bahati mbaya muda hautoshi na michezo muhimu ni mingi mbele yetu hivyo wachezaji wanalazimika kurejea kwa ajili ya kuanza maandalizi yetu ambapo tumeingia kambini leo Jumatatu na Jumanne wataanza rasmi maandalizi," amesema.

Mara baada ya mchezo wa Mtibwa Sugar, Yanga watakuwa na kibarua kingine cha kuwakaribisha Medeama katika mchezo ambao utapigwa Desemba 20 Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.