Bandari FC kushiriki Mapinduzi Cup visiwani Zanzibar

KANDANDA Bandari FC kushiriki Mapinduzi Cup visiwani Zanzibar

Zahoro Mlanzi • 16:38 - 11.12.2023

Michuano hiyo hufanyika kila mwaka ikiwa ni katika shamrashamra za kusherehekea mapinduzi ya uhuru wa visiwa hivyo

Timu ya Bandari ya Kenya, ni miongoni mwa timu nne zitakazotoka nje ya Tanzania kwa ajili ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza Desemba 28 visiwani Zanzibar.

Michuano hiyo hufanyika kila mwaka visiwani humo ikiwa na lengo la kusherehea Mapinduzi ya visiwa hivyo ambavyo vinatimiza miaka 60 ya kuwa huru.

Mbali na timu hiyo, zingine ni URA ya Uganda, Vital'O ya Burundi na APR ya Rwanda.

Kutoka kwenye Ligi ya Tanzania Bara, mabingwa wa ligi hiyo, timu ya Yanga SC, Simba SC, Azam FC na Singida Fountian Gate zitashiriki wakiungana na bingwa mtetezi wa michuano hiyo msimu uliopita, timu ya Mlandege kutoka Zanzibar.

Mbali na Mlandege lakini pia timu za KVZ, Chipukizi na Jamhuri nao watawakilisha kutoka upande wa Tanzania visiwani.

Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya michuano ya msimu huu, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi Cup, Suleiman Mahmoud Jabir, amesema hiyo itakuwa ni moja kati ya michuano mikubwa na bora kushuhudiwa kutokana na aina ya timu ambazo wameziandaa kushiriki.

Amesema timu zote zimethibitisha kushiriki na kinachosubiriwa ni muda tu wa kuzigawa timu katika makundi kabla ya kuanza michuano.

"Tunatarajia kuwa na michuano bora sana msimu huu kwasababu kwanza tumeongeza timu lakini pia tumealika timu zenye ushindani kutoka nje," amesema.

Aidha amebainisha mechi zote katika michuano ya msimu huu zitachezwa katika Uwanja wa Amani.

Msimu uliopita, Mlandege ilivunja mwiko kwa timu za Zanzibar kutofanya vizuri kwenye michuano hiyo baada ya kuibuka na taji kwa kuifunga Singida FG katika mchezo wa fainali uliochezwa Januari 13.