Twiga Stars yasonga mbele kufuzu WAFCON 2024

© Kwa Hisani

KANDANDA Twiga Stars yasonga mbele kufuzu WAFCON 2024

Zahoro Mlanzi • 19:32 - 26.09.2023

Matokeo hayo yameifanya Twiga Stars sasa kusubiri mshindi kati ya Togo au Djibouti.

Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), imetinga raundi ya pili kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024 kwa kuitandika Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kushinda 2-0 katika muda wa kawaida.

Licha ya kushinda mabao hayo, Twiga Stars bado ilihitaji mabao zaidi ili kusonga mbele baada ya mchezo wa awali uliochezwa jijini Abdijan kufungwa mabao 2-0 na ndio maana imelazimika kupigiana mikwaju ya penalti.

Mchezo huo umepigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ambapo mabao ya Twiga Stars yamefungwa na Donisia Minja na Oprah Clement katika kipindi cha pili cha mchezo huo uliokuwa wa kuvutia kutokana na ushindani uliokuwepo.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, zilikuwa hazijafungana licha ya Stars kuonekana kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa.

Matokeo hayo yameifanya Twiga Stars sasa kusubiri mshindi kati ya Togo au Djibouti.

Baada ya ushindi huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa zawadi ya sh. milioni 10 kwa timu hiyo na benchi zima la ufundi.

Aliyetoa taarifa hiyo ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ambaye alikuwa uwanjani kushuhudia mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wengi.