Kocha Azam alia ubutu ufungaji mabao

KANDANDA Kocha Azam alia ubutu ufungaji mabao

Zahoro Mlanzi • 16:00 - 10.09.2023

Azam FC iliishinda AS Artar Solar ya Djibouti kwenye mchezo wa kirafiki, lakini kocha Youssouph Dabo hakuridhika na mwenendo wa ushambuliaji wa timu yake.

Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Artar Solar 7 ya Djibouti katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, Kocha wa timu ya Azam FC, Youssouph Dabo, amesema safu yake ya ushambuliaji inakosa ufanisi katika kufunga mabao.

Katika mchezo huo umepigwa jana usiku uwanjani Azam Complex, Chamazi, mabao ya Azam yalifungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' na Prince Dube huku bao pekee la Solar 7 likifungwa na kiungo wa Kimataifa wa Mali, Moussa Coulibaly.

Azam FC imecheza mechi hiyo ikiwa inajiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Fountain Gate wakati Solar 7 ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri, mchezo utakaopigwa Jumamosi katika uwanja huo huo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Dabo amesema wamekosa ufanisi katika kupachika mabao wavuni kwani walitengeneza nafasi nyingi za kufunga.

"Nitaendelea kuwafundisha wachezaji wangu ili wawe wanafunga mabao zaidi, kwa nafasi tunazotengeneza ilitakiwa tuwe na mabao zaidi ya manne," amesisitiza Dabo.

Kwa upande wa Kocha wa Solar 7, Bouziane Benaraïbi, amesema wameridhishwa na matokeo waliyoyapata katika mchezo huo wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya Zamalek.

"Sina tatizo na matokeo dhidi ya Azam ila kiwango walichokionesha si kama nilivyotaka, lakini nitajua wapi kwa kuanzia kuelekea mchezo huo wa kimataifa," amesema Benaraïbi.

Tags: