Benchikha aahidi mambo mazuri mechi na ASEC Mimosas

KANDANDA Benchikha aahidi mambo mazuri mechi na ASEC Mimosas

Na Zahoro Juma • 22:00 - 22.02.2024

Kocha huyo wa Simba SC, ataiongoza timu yake katika mchezo ambao wanahitaji ushindi au sare kuniweka katika nafasi ya kusonga mbele

Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, ameahidi atapata matokeo mazuri kesho katika mechi yao ya ugenini dhidi ya Asec Mimosa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny nchini Ivory Coast kuanzia saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kubanwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza timu hizo zilipokutana Novemba, mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa raundi ya tano hatua ya makundi, Asec wao wanaingia wakiwa ni vinara wa Kundi B baada ya kukusanya alama 10 katika mechi zao nne zilizopita na tayari wameshakata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali.

Hata hivyo habari ni tofauti kwa Simba ambao wanahitaji zaidi alama katika mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele kwenda hatua ya robo fainali.

Akizungumza kwenye mkutano na wana habari leo, Kocha Benchikha, amesema wanatambua vyema umuhimu wa ushindi katika mchezo huo na ndio maana wamefanya maandalizi kwa ajili ya kufanya vizuri.

"Kila mchezo ni muhimu lakini tunatambua umuhimu wa kipekee wa mchezo huo wa kesho na hiyo ndio sababu imefanya tujiandae kwa ajili ya kufanya vizuri," amesema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na nahodha wake, Mohamed Hussein 'Tshabalala', ambaye amesema watafanya kila jitihada ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika mchezo huo ambao utachezwa saa 1 usiku kwa saa za Ivory Coast.

Simba hawana kumbukumbu nzuri kwani mara ya mwisho walipocheza ugenini dhidi ya Asec walikubali kichapo cha mabao 3-0 msimu wa 2021-22.

Katika mchezo huo, Simba inatarajia kuwakosa baadhi ya nyota wao wa kikosi cha kwanza akiwemo Kipa, Ayoub Lakred ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano huku pia wakimkosa Willy Onana ambaye alisalia nchini kutokana na majeraha ya mguu.