Rais Yanga afunguka mipango kuiua CR Belouizdad

Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said (kushoto), akishukuru baada ya kisaini mkataba

KANDANDA Rais Yanga afunguka mipango kuiua CR Belouizdad

Na Zahoro Juma • 20:02 - 22.02.2024

Ni kuelekea mechi ya Jumamosi ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Timu ya Yanga SC, inaingia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad Jumamosi lakini kichwani wakiwa na wazo moja tu la kuweka rekodi mpya katika michuano hiyo.

Tofauti na ilivyo kwa watani zao wa jadi, timu ya Simba ambao wameingia mara tatu katika hatua ya robo fainali, Yanga wao hawajawahi kufika hatua hiyo hata mara moja.

Mchezo huo dhidi ya vigogo hao kutoka Algeria ni muhimu kwao kusaka ushindi ili kuweka hai matumaini hayo.

Yanga wakiwa katika nafasi ya tatu na CR Belouizdad kwenye nafasi ya pili hadi sasa wote wana alama t5 kwenye msimamo wa Kundi D lakini kinachowatofautisha ni uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kuelekea mchezo huo, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema mipango yote imekamilika na wanalenga kwenda kuvuna alama tatu muhimu Jumamosi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa udhamini na Kampuni ya Karimjee Mobility ambao ni watengenezaji wa pikipiki za Hero, Hersi amesema kwa upande wa viongozi kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa hadi sasa kilichobaki ni jukumu la wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

"Mkataba huu umekuwa kama sehemu ya hamasa kuelekea mechi yetu muhimu ya Jumamosi, sisi kama viongozi tumefanya kila aina ya mahitaji ambayo tulipaswa kutumiza na jukumu tumelibakisha kwa wachezaji ambapo tunaamini kwamba tutafanya vizuri," amesema.

Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Algeria, Yanga ilikubali kichapo cha mabao 3-0.

Mbali na rekodi ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza lakini pia Yanga wanalenga kulipiza kisasi kwa kipigo hicho ambacho walikutana nacho katika mchezo wa kwanza tu wa hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa msimu huu.

Yanga na Karimjee Mobility kupitia bidhaa yao ya pikipiki ya Hero, zimeingia mkataba wa miezi 18 wenye thamani ya shilingi milioni 300.