Aucho wa Yanga afungiwa mechi tatu Ligi Kuu

KANDANDA Aucho wa Yanga afungiwa mechi tatu Ligi Kuu

Na Zahoro Mlanzi • 18:30 - 17.11.2023

Khalid Aucho amefungiwa mechi hizo na faini ya shilingi Tsh500,000 kutokana na utovu wa nidhamu aliouonesha Novemba 8

Kiungo wa timu ya Yanga SC, Khalid Aucho ambaye ni raia wa Uganda, amefungiwa kucheza mechi tatu na kutozwa faini ya shilingi Tsh500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union, Ibrahim Ajib.

Tukio hilo lilitokea Novemba 8 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya wenyeji Coastal Union walioikaribisha Yanga, mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Katika mchezo huo, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Clement Mzize.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, katika kikao chao cha Novemba 14 ndio kilifikia uamuzi huo.

Taarifa hilo imeeleza, Mwamuzi ambaye alichezesha mchezo huo, Emmanuel Mwandembwa, amefungiwa kuchezesha mechi za mashindano kwa kipindi cha miezi 6 kutokana na kushindwa kuumudu mchezo.

Lakini pia kamati hiyo haikuishia hapo, pia imetoa adhabu kwa beki wa timu ya Simba SC, Henock Inonga ametozwa faini ya shilingi Tsh500,000 kwa kosa la kushangilia mbele ya benchi la Yanga wakati wa mchezo wa ligi kuu baina ya timu hizo.

Adhabu kama hiyo imekwenda pia kwa kipa wa Yanga, Djigui Diarra ambaye naye alifanya kosa kama hilo kwenda kushangilia kwenye benchi la Simba.

Pia straika wa Simba, Kibu Denis ametozwa faini ya Tsh500,000 kwa kwenda kushangilia upande wa mashabiki wa Yanga huku akionesha ishara ya kuwaziba midomo.