Straika mpya Yanga SC aahidi mabao

KANDANDA Straika mpya Yanga SC aahidi mabao

Na Zahoro Juma • 18:19 - 31.01.2024

Ni yule nyota wa kimataifa wa Ivory Coast aliyesajiliwa akitokea Tuzlaspor ya Uturuki akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake

Mshambuliaji mpya wa timu ya Yanga SC raia wa Ivory Coast, Joseph Guede, amesema mashabiki wa timu hiyo watarajie makubwa kutoka kwake kuanzia mechi za Ligi Kuu ambazo zinatarajia kurejea hivi karibuni.

Hayo ameyazungumza muda mfupi baada ya kutambulishwa rasmi wakati wa mchezo wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Hausang kutoka Njombe.

"Nimekuja hapa kufanya kazi, sina ninachoweza kuwaahidi wananchi zaidi ya kufanya vizuri na kuisaidia timu kufikia malengo yake msimu huu," amesema Guede.

Guede alikamilisha usajili wa kujiunga na Yanga siku ya mwisho ya dirisha dogo la usajili ambalo lilifungwa Januari 15.

Katika hatua nyingine, kikosi kamili cha Yanga, kitaondoka jijini Dar es Salaam kesho kwenda mkoani Kagera tayari kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar unaotarajiwa kuchezwa Ijumaa Uwanja wa Kaitaba.

Akizungumza na Pulsesports jijini Dar es Salaam, Meneja wa Yanga, Walter Harrison, amesema wachezaji wote ambao wamerejea kutoka katika timu za taifa hasa Tanzania na Zambia wanatarajia kuwa sehemu ya msafara wa kikosi hicho.

Ameongeza hata mshambuliaji wao mpya Guede atakuwa sehemu ya kikosi na kama kocha ataamua basi ataweza kumtumia kwani tayari alishafanya mazoezi kwa siku kadhaa tangu alipotua nchini.

Wakati huo huo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema watakabiliana na ratiba ngumu ya ligi inayotarajia kuanza mwezi huu kwa kucheza na Kagera Sugar.

Gamondi amesema licha ya ugumu wa ratiba hiyo lakini amejiandaa kukabiliana nayo na atatoa nafasi kwa wachezaji wengi ili kuepusha uchovu na majeraha.

Yanga inatarajia kucheza michezo mitatu ndani ya siku 10 zijazo ikiwa ni mchezo mmoja kila baada ya saa 48.