Sillah, Sidibe waanza mazoezi Azam FC

Beki wa kushoto wa Azam FC, Cheikh Sidibe, akiwa mazoezini

KANDANDA Sillah, Sidibe waanza mazoezi Azam FC

Zahoro Juma • 16:30 - 30.01.2024

Nyota hao walikuwa majeruhi kwa muda mrefu na kukosa baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na Mapinduzi Cup

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah pamoja na mlinzi wa pembeni wa timu hiyo, Cheikh Sidibe, wamerejea mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya kukabiliana na Simba mchezo utakaopigwa Februari 9.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu hiyo, wachezaji hao wawili walikuwa wanakabiliwa na majeraha yaliyowafanya kutoonekana uwanjani kwa muda ikiwemo kukosa baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara na hata michuano ya Mapinduzi Cup.

Kurejea kwa wachezaji hao ambao walikuwa ni sehemu ya kikosi cha kwanza kabla ya kuumia itakuwa ni habari njema kwa benchi la ufundi la Azam chini ya Kocha, Yusuph Dabo.

Wawili hao wote ni maingizo mapya ndani ya Azam ambao walisajiliwa mwanzo wa msimu na walifanya vizuri katika mechi walizocheza ikiwemo kuifanya timu yao kuwa tishio kabla ya kupata majeruhi yaliyowalazimu kakaa nje.

Azam kwasasa ni vinara wa ligi hiyo wakiwa na alama 31 na wameshuka dimbani mara 13 katika mchuano hiyo.

Kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba ambao ni wa kiporo, Azam pia itakuwa na uhakika wa kuwatumia wachezaji wao wapya watatu ambao ni Kipa, Mustapha Mohamed, beki Yeison Fuentes na mshambuliaji Franklin Navarro ambao wote ni wa kimataifa na walisajiliwa katika dirisha dogo la usajili.

Katika hatua nyingine, timu ya Azam, itashuka uwanjani kesho kucheza na KVZ ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa saa 10.30 jioni Uwanja wa Azam Complex ule wa nyasi halisi bila ya kuwa na mashabiki.