Makocha Simba SC, Al Ahly wapigana mkwara

© Kwa Hisani

KANDANDA Makocha Simba SC, Al Ahly wapigana mkwara

Zahoro Mlanzi • 19:00 - 19.10.2023

Kocha wa Simba SC, Robert Oliviera, na wa Al Ahly, Marcel Koller, wajiandaa kwa mchezo wa ufunguzi wa michuano ya AFL nchini Tanzania.

Makocha wa timu za Simba SC, Robert Oliviera na wa Al Ahly, Marcel Koller, kila mmoja ametamba kufanya vizuri katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya AFL utakaopigwa kesho Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utaanza saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Ni mchezo wa kihistoria kufanyika katika ardhi ya Tanzania kutokana na uzito wa maandalizi yake pamoja na ugeni uliofika kushuhudia mchezo huo.

Kuelekea mchezo huo, Robertinho, amesema hana kawaida ya kuzungumza sana kabla ya mechi badala yake anawataka watu kushuhudia ambacho kitatokea uwanjani ndani ya dakika 90.

Hadi sasa taarifa zinaeleza kuwa tiketi zote zimeshauzwa.

Robertinho amesema Simba ni timu bora na kubwa barani Afrika na wanawaheshimu wapinzani wao hivyo wapinzani wao inabidi wawe na heshima kwao.

"Mimi huwa sio muumini wa kuongea sana kabla ya mechi majibu yangu huwa nayatoa ndani ya uwanja kwenye dakika 90," amesema Robertinho.

Aidha Robertinho amekiri kuhusu ugumu wa mpinzani wao kutokana na uzoefu walionao kwenye michuano mbalimbali lakini wao kama timu wamepata muda mwingi wa kujiandaa na kwamba malengo yao ni kufanya vizuri.

Kocha huyo raia wa Brazil, pia amezungumzia kikosi chake ambapo licha ya kuwa mlinzi wao tegemezi Mkongo, Henock Inonga kuchelewa kurejea lakini bado yupo kwenye mipango ya kikosi kitakachocheza leo.

Kwa upande wake, Kocha wa Al Ahly, Koller, amesema wanahitaji kufanya vizuri kwenye mchezo huo na ndio maana wamesafiri na kikosi chao kamili.

Simba na Al Ahly wanakutana kwa mara ya kwanza kwenye michuano hii mipya ambayo kesho ndio inazinduliwa rasmi mbele ya viongozi mbalimbali wa soka duniani akiwemo Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa CAF, Patrice Motsepe.

Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallec Karia, amezungumzia kuhusu ugeni ambao unatarajiwa kutua nchini kwaajili ya ufunguzi wa michuano hiyo ukiongozwa na Infantino ambaye atakuwa sambamba na Motpese.

Ameongeza wageni hao (Infantino na Motsepe) watakuwa na safari ya kwenda Dodoma kuonana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kisha kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya zoezi la kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa unaoendelea wa Kituo cha Kukuzia vipaji cha Kigamboni, ambacho kinajengwa na TFF chini ya ufadhili wa FIFA.

Mbali na mechi hiyo, mechi nyingine zilizobaki katika hatua hiyo ya robo fainali ni TP Mazembe vs Esperence de Tunis. Mchezo huu pia utachezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Nyingine ni Petro de Luanda ya Angola dhidi ya Mamelod Sundowns kutoka Afrika Kusini. Na mechi ya mwisho ni Enyimba ya Nigeria dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.