Rais Infantino kushuhudia mechi ya Simba, Al Ahly

© Kwa Hisani

KANDANDA Rais Infantino kushuhudia mechi ya Simba, Al Ahly

Zahoro Mlanzi • 13:09 - 12.10.2023

Infantino anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ukarabati wa uwanja huo ambao hivi karibuni Waziri wa Utamaduni.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA), Gianni Infantino, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Simba SC na Al Ahly wa michuano ya African Football League (AFL), utakaopigwa Oktoba 20, mwaka huu Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu ujio wa viongozi mbalimbali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Iman Kajula, amesema mbali na Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe pia atakuwepo na marais wa vyama vya soka vya nchi zingine.

Amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ukarabati wa uwanja huo ambao hivi karibuni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema ukarabati umefikia asilimia 95.

“Tunaishukuru serikali kwa matengezo makubwa ambayo imefanya kwenye Uwanja wa Mkapa. Simba pia imetoa mchango kiasi kufanikisha hili,” amesema Kajula.

Pia Kajula amezungumzia manufaa makubwa ya uwepo wa michuano hiyo nchini kwa kusema kutakuwa na fursa mbalimbali zitazopatikana kupitia michuano hiyo.

Amesema Tanzania inapaswa kujivunia kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa AFL.

“Licha ya kwamba ni tukio la siku moja, ila lina faida kubwa sana, kuna watu watatoka maeneo mbalimbali, kuna watakaotoka mikoani kwahiyo hiyo itakuwa pia fursa kwa wanaotaka kusafirisha mashabiki kuja Dar es salaam,”amesema Kajula

Kwa upande wa Ofisa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally, amezungumzia viingilio katika mchezo huo ambapo cha chini ni sh. 7,000 huku cha juu kikiwa ni sh. 200,000 kwa viti vya Platnum.

Amesema viti vya rangi ya machungwa ni sh. 10,000, VIP C ni sh. 30,000, VIP B ni sh. 40,000.