Azam FC yaipiga Chipukizi 1-0 Mapinduzi Cup

KANDANDA Azam FC yaipiga Chipukizi 1-0 Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 08:28 - 31.12.2023

Ushindi huo umeifanya Azam kukakaa kileleni ikiwa na alama nne katika Kundi A

Mshambuliaji wa timu ya Azam FC, Allasane Diao, aliifungia bao pekee timu yake na kuipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Chipukizi katika muendelezo wa mechi za michuano ya Mapinduzi Cup visiwani Zanzibar.

Katika mchezo huo wa Kundi A, Diao alifunga bao hilo mapema kipindi cha kwanza dakika ya 12.

Ushindi huo, umeifanya Azam kufikisha alama nne, wakikaa kileleni kwenye msimamo wa kundi hilo huku Vital'O na Mlandege wote wakiwa na alama mbili na Chipukizi wakiwa mkiani na alama yao moja.

Katika mchezo huo, mchezaji wa Azam, Diao alitajwa kuwa Mchezaji Bora wa mechi na kukabidhiwa kitita cha Tsh500,000 na wadhamini wa tuzo hiyo Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Kupitia mchezo huo, Kocha wa Azam, Yusuph Dabo, alimpa nafasi mshambuliaji mpya wa timu hiyo, raia wa Colombia, Franklin Navarro ambaye alitangazwa kusajiliwa siku mbili mbili zilizopita.

Kabla ya mchezo huo, Vital'O na Mlandege walitoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo ambao ulichezwa mapema.

Michuano hiyo inaendelea leo na kutakuwa na michezo miwili ambapo saa 10 kutakuwa na mechi kati ya KVZ na Jamus wakati usiku kutakuwa na mechi kati ya Yanga na Jamhuri.

Tags: