Azam FC yaanza na suluhu Mapinduzi Cup

KANDANDA Azam FC yaanza na suluhu Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi • 19:17 - 28.12.2023

Mchezo huo ulikuwa ni wa kwanza katika michuano ya msimu huu ambapo timu hizo zimegawana pointi

Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Azam FC, imefungua pazia la michuano ya Mapinduzi Cup msimu huu kwa kulazimishwa suluhu na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, timu ya Mlandege FC.

Mchezo huo wa ufunguzi ulichezwa katika dimba la New Amani Complex, Zanzibar ikiwa ni mchezo wa pili kufanyika hapo tangu uwanja huo ulipozinduliwa baada ya maboresho Desemba 27.

Azam ambao ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa michuano hiyo, ilipanga kikosi chenye nyota mchanganyiko wakiwemo wachezaji wao tegemeo Prince Dude, Allasane Diao, Yannick Bangala, Edward Manyama, Ayoub Lyanga na James Akaminko.

Hata hivyo licha ya kuwa na nyota wote hao uwanjani lakini Mlandege walionekana kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuibuka na ushindi kama sio mshambuliaji wao Idd Pina kupoteza nafasi nyingi za kufunga hasa kipindi cha kwanza.

Katika mchezo huo, mchezaji wa Azam, Bangala alizawadiwa Tsh500,000 na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Mlandege, Hassan Ramadhan, amesema huo ni mwanzo tu lakini watajitahidi kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo ili kutetea ubingwa wao.

"Najivunia wachezaji wangu wamecheza vizuri hasa ukiangalia aina ya timu ambayo tumecheza nayo, hivyo naamini mechi zijazo tutapata ushindi ambao utafanya tuibuke na taji msimu huu," amesema.

Kwa upande wa Kocha wa Azam, Yusuph Dabo, aliwasifu Mlandege kwa mchezo mzuri walioonesha na aliahidi kufanya vizuri katika mechi yao inayofata.

Azam watashuka tena dimba Desemba 30 kucheza na Chipukizi wakati huo Mlandege wao watakabiliana na Vital'O ya Burundi siku hiyo.

Tags: