Simba SC yazindua jezi mpya za kimataifa

KANDANDA Simba SC yazindua jezi mpya za kimataifa

Zahoro Mlanzi • 16:04 - 22.11.2023

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ambapo kama kawaida wametoa jezi za aina tatu yaani nyekundi, nyeupe na ya bluu

Klabu ya soka ya Simba, imezindua jezi zao mpya ambazo watazitumia kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia hatua ya makundi.

Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam ambapo kama kawaida kwa kutoa jezi za aina tatu yaani nyekundi, nyeupe na ya bluu.

Simba wanatarajia kuanza kibarua cha michezo hiyo ya kimataifa dhidi ya Asec Mimosa ya Ivory Coast.

Mchezo huo utachezwa Jumamosi kuanzia saa 10 jioni Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya uzinduzi huo, mashabiki na wadau wa soka, wametoa maoni kutokana na muonekana wa jezi hizo yaliyoonekana kukinzana.

Mmoja wao aliandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X wa klabu hiyo: "Jezi nzuri ila zina logo mbili za Mo xtra sijui kwanini imekuwa hivyo, matangazo mengi."

Kuelekea mchezo huo wageni Asec wanatarajia kuingia nchini leo wakiwa na kikosi chao kamili kwa ajili ya kipute hicho.

Timu hizo kila mmoja sio mgeni kwa mwenzie kwani misimu miwili nyuma walipangwa katika kundi moja ambapo katika mechi ya Dar es Salaam, Simba walishinda mabao 3-1 na katika mchezo uliochezwa ugenini, wenyeji Asec walishinda 3-0.

Simba wataingia katika mchezo huu huku swali kubwa ambalo linaumiza vichwa vya watu ni kuhusu suala la nani atakuwa kocha wa timu hiyo.

Kwasasa timu ipo chini ya Kocha, Daniel Cadena ambaye anatarajia kuiongoza katika mchezo wa kwanza dhidi ya Asec.

Mara baada ya mchezo huu Simba ambao wapo Kundi B, itafunga safari kwenda Botswana kwa ajili ya kukabiliana na Jwaneng Galaxy, mchezo ambao utapigwa Desembe 2.