Singida FG yaacha nyota wake sita

Beki kisiki raia wa Kenya, Joash Onyango, ni miongoni mwa wachezaji walioachwa

KANDANDA Singida FG yaacha nyota wake sita

Na Zahoro Juma • 20:39 - 18.01.2024

Hatua hiyo imetokana na timu hiyo yenye maskani yake mkoani Singida kuboresha vitabu vyao vya kimahesabu

Klabu ya Singida FG, imetangaza kuachana na nyota sita ambao walikuwa wanaunda kikosi cha kwanza na taarifa zinadai kuwa huenda wakatimkia katika timu ya Ihefu ya mkoani Mbeya.

Nyota hao ni Morice Chukwu, Joash Onyango, Khomeiny Abuubakar, Duke Abuya na Marouf Tchakei.

Awali pia Singida FG wametangaza kumuachia Meddie Kagere aliyejiunga na Namungo ya Lindi huku pia nahodha wao, Gadiel Michael akijiunga na timu ya Cape Town Spurs ya nchini Afrika Kusini.

Katika hatua zote hizo za kuachia wachezaji, Singida FG haijatangaza kununua mchezaji yeyote katika usajili wa dirisha dogo ambao ulifungwa tangu Januari 15.

Vyanzo mbalimbali vya habari nchini Tanzania, vimedai huenda timu hiyo inakabiliwa na ukata kwasasa kitu ambacho Rais wa timu hiyo, Japhet Makau alikanusha mapema wiki hii.

"Hatuna tatizo lolote la fedha ila tupo katika hali ya kuboresha vitabu vyetu vya kimahesabu," amesema.

Singida FG ambao msimu huu walishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na waliondoshwa na Klabu ya Future FC ya nchini Misri.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu hiyo ipo nafasi ya tano baada ya kucheza mechi 14 na kukusanya alama 20.

Tags: