Simba SC kutesti mitambo kesho na TRA Kilimanjaro

KANDANDA Simba SC kutesti mitambo kesho na TRA Kilimanjaro

Na Zahoro Juma • 17:34 - 27.02.2024

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi kujiandaa na mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy

Kikosi cha timu ya Simba SC, kimeingia katika mawindo rasmi ya kuzisaka alama tatu dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana Jumamosi baada ya wachezaji kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Hata hivyo kuelekea mchezo huo, kesho Simba itashuka dimbani kucheza mechi ya kiporo ya michuano ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya TRA Kilimanjaro ambapo kwa mujibu wa uongozi wamebainisha itakuwa ni kama mechi ya kupasha misuli.

Simba inahitaji kuibuka na ushindi wowote Jumamosi dhidi ya Jwaneng ili iweze kukata tiketi ya kucheza robo fainali kwa mara ya nne mfululizo.

"Tunaitaka robo fainali na ndio maana mapema tu baada ya kurudi Dar es Salaam wachezaji wameanza maandalizi kuelekea mchezo wa Jumamosi, hata hivyo kesho tutakuwa na mchezo wa FA ambapo tutautumia kwa ajili ya kujiweka sawa," amesema Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.

Katika mchezo wa Jumamosi licha ya kuwa watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Benjamini Mkapa lakini mechi hiyo haitarajiwi rahisi kwa upande wa Simba wala Jwaneng ambao nao bado wanayo nafasi ya kusonga mbele.

Msimamo wa Kundi B unaonesha kuwa Asec Mimosas ya Ivory Coast wao wameshafuzu kwenda robo fainali wakiwa vinara baada ya kukusanya alama 10 na wanafuatiwa na Simba kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama sita sawa na Wydad Casablanca huku Jwaneng wakiburuza mkia na alama nne.

Kuelekea mchezo huo, uongozi wa Simba ulibainisha wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-1 walichopata kutoka kwa Jwaneng, Oktoba 24, 2021 na watatumia mchezo huo kama sehemu ya kulipa kisasi.

Kama ikitokea Simba wakikata tiketi hiyo ya robo fainali basi itakuwa imetengeneza historia nyingine mpya kwa soka la Tanzania kuwa na wawakilishi wawili katika hatua hiyo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Yanga kutangulia.

Tags: