Simba Queens, Yanga Princess kuumana Jan. 3 Ligi Kuu Wanawake

KANDANDA Simba Queens, Yanga Princess kuumana Jan. 3 Ligi Kuu Wanawake

Zahoro Mlanzi • 20:39 - 28.11.2023

Ligi hiyo itaanza rasmi Desemba 20 kwa bingwa mtetezi, JKT Queens kuumana na Bunda Queens

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza ratiba ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara 2023/24 ambapo Simba Queens itaumana na Yanga Princes Januari 3, mwakani.

Bingwa mtetezi wa ligi hiyo ni JKT Queens ambaye alipata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, michuano iliyomalizika mwezi huu nchini Morocco na Mamelodi Sundown Ladies kutwaa ubingwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, ligi hiyo itaanza rasmi Desemba 20 ambapo mabingwa watetezi, JKT Queens itafungua dimba kwa kuumana na Bunda Queens.

Mbali na mechi hiyo lakini kutakuwa na mechi nyingine nne za mzunguko wa kwanza ambapo Simba Queens itaumana na Ceasia Queens huku Allience Girls wakianza na Geita Gold Queens, Foutaine Gate Queens wao watacheza na Amani Queens na mechi zote hizi zitapigwa siku ya ufunguzi.

Mchezo wa mwisho kwa raundi ya kwanza utapigwa Desemba 21 ambapo Baobao Queens watawaalika Yanga Princess katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Macho na masikio ya wengi yataelekezwa katika mechi ya Kariakoo Dabi kwa upande wanawake ambapo Januari 3, Simba Queens watakuwa ni wenyeji wa Yanga Princess.

Mchezo huo unatarajia kuvuta hisia za watu wengi wa soka nchini hasa ukikumbuka matokeo ya kichapo cha mabao 5-1 walichopata Simba kutoka kwa Yanga katika mechi za timu za wanaume.

Wawili hao watarudiana tena Machi 22 mwakani ambapo Yanga Princess watakuwa wenyeji katika mchezo huo.

Ligi hiyo inatarajia kufika tamati Mei 17 ambapo Yanga Princess watafunga dimba dhidi ya Alliance huku Simba Queens wakifunga dimba na Geita Gold Queens.

Tags: