Minziro awa kocha wa 7 kutimuliwa Ligi Kuu

KANDANDA Minziro awa kocha wa 7 kutimuliwa Ligi Kuu

Na Zahoro Mlanzi • 18:34 - 21.11.2023

Timu zingine zilizowahi kutimua makocha wake kabla ya mzunguko wa kwanza haujaisha ni Simba SC, Namungo FC, Ihefu FC, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Singida Fountain Gate.

Kocha Fredy Felix 'Minziro', amekuwa kocha wa saba kutimuliwa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2023/24 baada ya kusitishiwa mkataba na Tanzania Prisons.

Uongozi wa Prisons, umefikia hatua hiyo baada ya kocha huyo kutokuwa na mwenendo mzuri katika ligi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mtandao wa kijamii wa Tanzania Prisons, kwa sasa timu hiyo itakuwa chini ya Kocha msaidizi, Shaban Mtupa hadi watakapotangaza kocha mwengine.

Kikosi cha Prisons hakikuanza vizuri msimu huu ambapo katika michezo 9 iliyocheza hadi sasa imevuna alama 7.

Mchezo wao wa mwisho kabla ya mapumziko kupisha timu za taifa, walikumbana na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Kagera Sugar.

Minziro ambaye ni mchezaji na Kocha wa zamani wa Yanga, alijiunga na Prisons mwanzoni mwa msimu huu akitokea katika Klabu ya Geita Gold na aliingia hapo kuchukuwa nafasi ya Mohamed Baresi ambaye alijiunga na Mashujaa FC.

Akizungumza na Pulse Sports kuhusu kutimuliwa kwake, Minziro, amesema licha ya kusitishiwa mkataba lakini ameiacha timu ikiwa katika morali ya juu.

"Kwasasa sijajua wapi nitaelekea ila ninachosubiri ni kuona nikilipwa stahiki zangu kwanza," amesema Minziro.

Prisons sasa inaungana na timu za Simba SC, Namungo FC, Ihefu FC, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Singida Fountain Gate ambayo imetimua makocha mara mbili kabla ya mzunguko wa kwanza kumalizika.

Tags: