Kocha Twiga Stars apania kufuzu WAFCON 2024

KANDANDA Kocha Twiga Stars apania kufuzu WAFCON 2024

Na Zahoro Mlanzi • 16:30 - 03.12.2023

Timu hiyo itaingia uwanjani ikitoka kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Togo, hivyo matokeo mazuri ya mchezo huo wa marudiano yataifanya kufuzu kwa fainali hizo

Kocha wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars', Bakari Shime, amesema wataenda kupambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kufuzu kwa fainali za WAFCON mwakani nchini Morocco.

Twiga Stars imeondoka nchini Tanzania ikiwa na faida ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Chamazi Complex, Dar es Salaam na zitarudiana Jumanne nchini humo.

Akizungumza na Pulsesports kabla ya kuanza safari, Kocha Shime amesema wanajua utakuwa mchezo mgumu ukizingatia wanacheza kwao, hivyo watapambana na wao kupata matokeo.

"Tunashukuru Mungu kila kitu kilienda sawa, tumefanya maandalizi mazuri na kilichobaki ni dakika 90 zingine za ugenini, tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," amesema Shime.

Ameongeza wanajua mchezo utakuwa mgumu kwakuwa wapinzani wao watataka kupindua meza, hivyo watacheza kwa tahadhari kubwa ili tufuzu kwa fainali hizo.

Kikosi hicho cha Twiga Stars kinaundwa na baadhi ya nyota ambao wanacheza soka la kulipwa akiwemo Oppa Clement anayecheza Uturuki katika Klabu ya Besiktas na ambaye ndio alifunga mabao mawili katika mechi ya kwanza.

Wengine ni Diana Lucas anayecheza katika Klabu ya Ausfaz Assa Zag ya nchini Morocco, Enekia Kasonga anayecheza nchini Saudi Arabia katika Klabu ya Eastern Flames na Aisha Masaka anayecheza nchini Sweden katika Klabu ya BK Hacken.

Kama Twiga Stars itafuzu, itaungana na timu taifa ya Wanaume 'Taifa Stars' ambayo imeshakata tiketi ya kucheza fainali za AFCON mwakani nchini Ivory Coast.

Tags: