Aziz KI awa Mchezaji Bora Oktoba ndani ya Yanga SC

Ligi Kuu Aziz KI awa Mchezaji Bora Oktoba ndani ya Yanga SC

14:07 - 29.10.2023

Tuzo hiyo inatolewa ndani ya Yanga ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kuingia mkataba na NIC wa miaka mitatu wenye thamani ya sh. milioni 900 za Kitanzania

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephan Aziz KI, ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Oktoba ndani ya timu yake.

Aziz Ki ameshinda tuzo hiyo akiwazidi Max Nzengeli na Dickson Job ambao aliingia nao Tatu Bora.

Tuzo hiyo ni mara ya kwanza kutolewa ndani ya Yanga mara tu baada ya kuingia mkataba na Kampuni ya Bima ya Taifa (NIC) ambao wameweka sh. milioni 900 kudhamini tuzo hiyo kwa miaka mitatu.

Mbali na tuzo lakini Aziz Ki anatarajiwa kupokea kiasi cha fedha taslimu sh. milioni 4 ikiwa ni zawadi ya mshindi kwa kila mwezi.

Mwezi Oktoba ulikuwa ni mzuri kwa Aziz Ki ambaye aliisaidia timu yake kupata ushindi kwenye michezo mitatu kati ya minne walioshuka dimbani huku yeye akifunga mabao manne.

Kumbuka ndani ya Oktoba ni kiwango chake alichoonesha wakati Yanga wakiwaburuza Azam kwa mabao 3-2 huku Aziz Ki akifunga mabao yote matatu 'Hat trick'.

Kwa upande wa Max, ndani ya Oktoba yeye amefunga mabao matatu huku Job ambaye ni mlinzi wa kati hakufunga bao lolote.

Tuzo hizo huamuliwa na mashabiki ambao hupewa fursa ya kupiga kura kupitia App za Yanga na matokeo yake hutangazwa baada ya mwezi kukamilika.

Tags: