Yanga yaja na 'Key day' kuivaa Marreikh

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga yaja na 'Key day' kuivaa Marreikh

Zahoro Mlanzi • 21:34 - 26.09.2023

Yanga itaumana na Merreikh Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mchezo wa mkondo wa pili kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu ya Al-Merreikh ya Sudan, ikitarajiwa kutua nchini Tanzania kesho mchana, wenyeji wao, timu ya Yanga SC, wamezindua rasmi kauli mbiu ya 'Key day' kuelekea mchezo huo.

Yanga itaumana na Merreikh Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mchezo wa mkondo wa pili kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa awali uliopigwa Rwanda, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Ally Kamwe, amesema wamesikia kauli za Kocha wa Al-Merrikh aliyesema timu yao inaogopeka Afrika.

"Sisi tumesoma Cuba, tunamwelewa, hawezi kutuchota, tutauchukulia mchezo wetu wa pili kwa umakini mkubwa," amesema Kamwe.

Amesema wana mpango wa kuja kucheza soka la kushambulia kitu ambacho kwao ni taarifa njema kwa sababu wana imani watafunga mabao mengi zaidi.

"Kimsingi sisi hatuna rekodi nzuri kucheza hatua ya makundi. Hilo halina siasa, ni uhalisia. Lakini kwa wakati huu tuna imani kubwa tutavunja huo mwiko. Dhamira yetu ni kubwa mno kuanzia kwa wachezaji hadi kwa mashabiki," amesema.

"Ukitaka kujua wana Yanga wana ugwadu na huu mchezo, tayari baadhi yao wameshaingia kwenye mfumo kuangalia tiketi, tayari baadhi ya mashabiki wameshanunua tiketi kupitia mfumo kabla ya sisi kutangaza mfumo hadharani."

Ameongeza msimu huu wamekuja kiutofauti kwa mechi zote za Kimataifa watazitangaza kwa jina la mchezaji kama ambavyo walifanya kwa Maxi Nzengeli na mchezo wao ujao utakuwa ni mtoko wa Stephano Aziz KI na kuwataka kila shabiki kuja uwanjani na funguo.

"Lazima tuwe na funguo ya kuingia mlango wa makundi ambao haujafunguka. Hii itaitwa Key day," amesisitiza Kamwe.