Beki Simba anusurika ajalini

©Kwa hisani

KANDANDA Beki Simba anusurika ajalini

Zahoro Mlanzi • 17:43 - 24.09.2023

Beki wa Simba SC, Che Malone Fondoh, amenusurika ajali baada ya gari lake kumkwepa mwendesha boda boda na kuingia mtaroni.

Beki wa timu ya Simba SC, Che Malone Fondoh, amenusurika ajalini baada ya gari yake kumkwepa mwendesha boda boda na kuingia mtaroni.

Fondoh ambaye ni raia wa kimataifa wa Cameroon, amesajiliwa na timu hiyo msimu huu akitokea Cotton Sports ya nyumbani kwako.

Akizungumzia ajali hiyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally, amesema Fondoh amepata ajali hiyo wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) alipokwenda kuwapokea ndugu zake.

"Amepata ajali akiwa njiani kwenda nyumbani kwake eneo la Mikocheni, kaka yake ndio kidogo aliumia na kwenda kufanyiwa vipimo hospitali na kuonekana hakuumia sana ambapo baadaye aliruhusiwa," amesema Ally.

Amesema Fondoh hakuumia kwani baada ya ajali hiyo alifanyiwa vipimo pamoja na ndugu zake wengine wawili aliokuwa nao katika gari yake na wote wameonekana wapo salama.

Amesema kikubwa aliwaomba wana-Simba kutulia kwani beki wao hajapata majeraha makubwa na Jumatatu wanatarajia kuingia kambini kujiandaa na mechi dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Simba inajiandaa kurudiana na Dynamos katika mchezo utakaopigwa Oktoba Mosi baada ya mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Zambia kutoka sare ya mabao 2-2.