Taifa Stars kuanza na Morocco AFCON 2024

KANDANDA Taifa Stars kuanza na Morocco AFCON 2024

Zahoro Mlanzi • 20:38 - 23.12.2023

Timu hiyo inacheza fainali zake za tatu tangu taifa hilo la Tanzania kupata uhuru

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars', inatarajia kutupa karata yake ya kwanza kwenye michuano ya Afcon kwa kucheza na Morocco, Januari 17.

Mchezo huo wa Kundi F, unatarajia kupigwa majira ya saa 11 kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Michuano hiyo inatarajia kuanza kutimua vumbi Januari 13 nchini Ivory Coast.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF),mara baada ya mchezo dhidi ya Morocco, Stars watashuka tena dimbani Januari 21 kucheza dhidi ya Zambia.

Stars watahitimisha michezo ya makundi kwa kucheza na DR Congo, Januari 24.

Washindi wawili wa kila kundi watapata nafasi ya kutinga hatua ya 16 Bora.

Kikosi cha Stars chini ya Kocha, Adel Amrouche kinatarajia kuingia kambini siku za hivi karibuni tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michuano hiyo.

Tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeshatuma orodha ya majina 54 ya kikosi cha awali kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Baada ya michezo ya leo ya Ligi Kuu Bara, ligi hiyo itasimama kupisha michuano ya Mapinduzi Cup pamoja na AFCON 2024.